WIZARA ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania, imewahakikishia usalama wa watalii wanaoingia nchini humo kutembelea utalii hawaathiriki na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19). Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).
Kauli hiyo ilitolewa juzi Jumapili tarehe 5 Julai 2020 na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda wakati wa uzinduzi wa wimbo uliotungwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RC), Anna Mghwira wa kumshukuru Mungu baada ya kumponya corona.
Profesa Mkenda alisema, tayari idadi ya watalii wanaoingia nchini inaongezeka tofauti na ilivyokuwa awali baada ya kuingia ugonjwa wa corona ambao ulisababisha kusitishwa kwa safari katika mataifa mbalimbali.
“Tanzania imechukua hatua kubwa sana na makini katika kupambana na ugonjwa wa corona na taratibu zote ambazo zimeelekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) la kuhakikisha usalama wa kila mgeni anayeingia nchini zimefwatwa hivyo tuwaondoe hofu wageni wetu, Tanzania iko salama,” alisema Profesa Mkenda.
“Kinachosababisha watalii wasije hapa sio kwamba wanaona tu kwamba huku kuna tatizo lakini kwa nchi zao kuna tatizo.”
“Kwanza wameathirika kiuchumi, wanahofu ya kusafiri kwenda nchi nyingine na wanatoa tahadhari kwa wananchi wao kusafiri wasipokuwa na uhakika kwamba nchi yetu imejipanga vizuri,” alisema Profesa Mkenda
Awali, akizungumzia wimbo huo, RC Anna alisema ameamua kutunga wimbo huo wa shukrani kwa Mungu kwa kumponya na corona baada ya kuambukizwa akiwa katika majukumu ya kuwatumikia wananchi.
Leave a comment