September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi mkuu 2020: Mrema asema mitego ya TLP haijakaa sawa

Spread the love

AUGUSTINE Lyatonga Mrema, Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), amesema mitego ya chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, bado haijakaa sawa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mrema amesema hayo leo Jumanne tarehe 7 Julai 2020, alipoulizwa na MwanaHALISI Online kwa simu, maandalizi ya TLP kuelekea uchaguzi huo wa urais, ubunge, uwakilishi na udiwani.

Mwenyekiti huyo wa TLP amesema, kwa sasa hawezi kuzungumzia maandalizi ya chama chake katika kushiriki uchaguzi huo, kwa kuwa mitego yao haijakaa sawa, hivyo wanasubiri vyama vya siasa alivyoviita vikubwa, viamue, kisha wao watafuata.

Hata hivyo, Mrema amesema TLP ilishafungua pazia kwa watia nia wa kugombea nafasi mbalimbali, kuchukua fomu, lakini mwitikio wao umekuwa mdogo.

Mrema amesema atatoa taarifa rasmi juu ya maandalizi ya uchaguzi huo, baada ya wiki moja kuanzia leo.

“Sisi bado mitego yetu haijakaa sawa, tunasubiri vyama vikubwa vimalize  ndio sisi tutafuata. Zoezi la kutafuta wagombea tumeshalianza ila waliojitokeza wachache,” amesema

“Kuhusu nini kinaendelea zaidi nitakupa taarifa baada ya wiki moja,” amesema Mrema.

Katika nyakati tofauti Mrema alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba, TLP itamuunga mkono Rais John Magufuli, katika uchaguzi wa urais wa Tanzania, kutokana na kukoshwa na utendaji kazi wake.

error: Content is protected !!