Friday , 26 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Papa amteua Askofu Nzigilwa, kuwa Askofu Mkuu jimbo la Mpanda
Habari Mchanganyiko

Papa amteua Askofu Nzigilwa, kuwa Askofu Mkuu jimbo la Mpanda

Askofu Eusebius Nzigilwa
Spread the love

BABA Mtakatifu, Francisko amemteuwa Askofu msaidizi, Eusebius Nzigilwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Mkoa wa Katavi. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Nzigilwa alikuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Maalumu … (endelea). 

“Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki Mpanda, alizaliwa tarehe 14 Agosti, 1966. Akapewa daraja Takatifu ya Upadre tarehe 23 Juni 1995. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, tarehe 28 Januari 2010 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kuwekwa wakfu tarehe 19 Machi 2010.”

Taarifa iliyotolewa na mtandao wa Kanisa hilo makao makuu Vatican, Roma nchini Italia leo Jumatano tarehe 13 Mei 2020 umesema Jimbo la Mpanda, limekuwa wazi tangu tarehe 21 Desemba 2018 baada ya Baba Mtakatifu, Francisko kuunda Jimbo kuu Jipya la Mbeya.

Jimbo hilo Kuu la Mbeya linaloongozwa na Askofu Mkuu, Gervas Nyaisonga, linalojumuisha, Jimbo la Mbeya, Jimbo la Iringa na Jimbo la Sumbawanga.

Kabla ya uteuzi huo wa Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda.

Kuteuliwa kwa Askofu Nzingilwa kuwa Askofu wa Jimbo la Mpanda kunamfanya, Askofu Mkuu, Yuda Thadeus Ruwa’ichi kubaki peke yake akiongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Askofu Nzigilwa, alizaliwa tarehe 14 Agosti, 1966, Jijini Mwanza nchini Tanzania.

Alipata masomo yake ya sekondari Seminari ndogo ya Mtakatifu Petro, Jimbo Katoliki la Morogoro.

Mnamo mwaka 1988 alishiriki katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria na baadaye, alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa masomo ya Falsafa na yale ya Taalimungu katika Seminari kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora.

Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 23 Juni, 1995 kama Padre wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

“Kwa hakika mwaka 2020 anatarajia kuadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya Upadre,” inaeleza taarifa hiyo.

Kuanzia mwaka 1995-1996 alikuwa ni Padre mlezi, nyumba ya malezi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, iliyoko Parokia ya Mtongani, Kunduchi.

Aliwahi pia kuwa ni Mkurugenzi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu kuanzia Mwaka 1996 hadi Mwaka 1997.

Baadaye Kardinali Polycarp Pengo alimteuwa kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Visiga, Jimbo kuu la Dar es Salaam kuanzia mwaka 1997-1999.

Baadaye akaendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikojipatia shahada ya kwanza ya elimu.

Baada ya masomo, aliteuliwa kwa mara nyingine tena na Kardinali Pengo kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Visiga, kuanzia 2003 hadi 2008 alipolazimika kwa mara nyingine tena kurudi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kumalizia masomo yake katika Sayansi ya Elimu na hivyo kujipatia Shahada ya uzamili.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!