MJI wa Hong Kong nchini China, leo Jumatano tarehe 13 Mei 2020, umeripoti wagonjwa wawili wapya wenye maambukizo wa virusi vya corona (COVID-19). Inaripoti Aljazeera…(endelea).
Mamlaka za jiji hilo zimeeleza, maambukizi hayo ni ya ndani (local transition), na yamethibitisha kwamba watu hao walioambukizwa, hawajakutana na watu wowote kutoka nje ya taifa ama jiji hilo.
Hatua hiyo imeshtua mamlaka za jiji hilo hasa kutokana na waathirika hao kutokuwa karibu ama kukutana na watu kutoka nje ya jiji ama taifa hilo.
Mamlaka za jiji hilo sasa zinaamini, maambukizo bado yapo mtaani ikiwa ni wiki moja baada ya kufungua shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na majumba ya sinema, majumba ya mazoezi na sehemu za vilevi (bar).
Kutokana na mafanikio ya awali, mamlaka za jiji hilo zilieleza mpango wake mpya wa kufungua shule mwishoni mwa mwezi huu wa Mei.
Hata hivyo, sasa zinafikiria upya. Zuio la kundi la watu wanaoanzia wanane, lipo palepale.
Jiji hilo ambalo ni muhimu kwa uchumi Asia na duniani kote, ni miongoni mwa majiji yaliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa kudhibiti ugonjwa huo pale ulipoanza kulipuka.
Ni jiji ambalo katika hatua za mwanzo kabisa, liliwaweka watu wake karantini na kutumia njia mbalimbali wanavikabili virusi hivyo ikiwa ni pamoja na sheria zingine zilizowekwa ili kufikia lengo.
Hata hivyo, taarifa ya kuwepo kwa maambukizi hayo, hasa tabu ya kufuatilia namna walivyopata maambukizi hayo watu hao, kumewaweka kwenye tahadhari kubwa kwamba, huenda mazingira yajayo yakawa magumu.
Leave a comment