January 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mvua Dar: 12 wapoteza maisha

Spread the love

WATU 12 wamefariki dunia jijini Dar es Salaam kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa  iliyonyesha tarehe 13 Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa ya vifo hivyo imetolewa leo tarehe 15 Oktoba 2020 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, SACP Lazaro Mambosasa, wakati akitoa tathimini ya athari ya mvua hiyo iliyosimamisha shughuli za jiji hilo Jumanne iliyopita.

Kamanda Mambosasa amesema vifo hivyo vilitokea katika Mikoa ya Kipolisi ya Kinondoni na Ilala jijini humo, ambapo watu nane walifariki dunia kwa kusombwa na maji.

Kamanda Mambosasa vifo nane vimetokea Ilala, amewataja marehemu hao kuwa ni, Mariam Yahaya (45) aliyekuwa Mkazi wa Vingunguti aliyesombwa na maji wakati akiokoa vyombo vyake.

“Mariam alifariki dunia baada ya kusombwa na maji wakati akijaribu kuokoa vyombo vyake vilivyokuwa vinasombwa na maji. Mwili wake ulikutwa unaelea kando ya mto Msimbazi na  umehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili,” ameeleza Kamanda Mambosasa.

Wengine walipoteza maisha Ilala ni, Herieth Kanuti (18) mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Lutihinda. Ipyana Mwakifuna, Mkazi wa Jangwani. Pamoja na watu wengine watatu  majina yao hayajafahamika, ambao wote watano miili yao iliokotwa kwenye Bonde la Mto Msimbazi.

Wengine waliopoteza maisha Ilala ni, Philipo Felician, mkazi wa Tabata Kimanga aliyepoteza maisha kwa kusombwa na maji baada ya kidondoka alipojaribu kuvuka Mto Tenge kupitia katika daraja la wapita kwa miguu. Mwili wake ulikutwa umenasa katika mto huo.

Mwili mwingine uliokotwa maeneo ya Ukonga wa mtu ambaye jina lake halijafahamika anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35.

Kamanda Mambosasa amesema vifo vinne vimetokea mkoa wa Kipolisi Kinondoni. Ambapo vifo vitatu vilitokea maeneo ya Kigogo baada ya Watoto wawili wa nyumba moja walifariki dunia baada ya nyumba yao kujaa maji na Ibrahim Hassani alifariki dunia alipojaribu kuwaokoa watoto hao.

“Watoto hao walifariki dunia kwa kusombwa na maji baada ya nyumba yao iliyopo katika Bonde la Kigogo kujaa maji na watoto hao kushindwa kujiokoa na marehemu Ibrahim Hassani  alijaribu kumuokoa mtoto mmoja lakini na yeye akasombwa na maji na kufariki dunia,” amesema Kamanda Mambosasa.

Kamanda Mambosasa amesema mwili mwingine uliokotwa katika maeneo ya Mambibo ukiwa mferejino kuelekea mto Msimbazi.

“Pia mnamo tarehe 14 Oktoba 2020 majira ya saa mbili asubuhi huko Mabibo mwili wa mtu mmoja mwanaume asiyefahamika  anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30-35  ulionekana unaelea kwenye mfereji unaopeleka maji katika mto Msimbazi.

Miili ya marehemu imehifadhiwa hospitali ya Taifa Muhimbili,” amesema Kamanda Mambosasa.

error: Content is protected !!