FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania Chadema ameshinda kura za maoni za kuwani Ubunge wa Hai Mkoa wa Kilimanjaro katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Hai … (endelea).
Mbowe amepigiwa kura za maoni jana Jumamosi tarehe 25 Julai 2020 na wajumbe wa mkutano mkuu wa Jimbo hilo uliofanyika ukumbi wa KKKT jimboni humo akiwa mgombea pekee wa nafasi hiyo.
Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Michael Kilawaila amesema, Mbowe alipigiwa kura 203 za ndio na mbili za hapana.
Aidha katika uchaguzi huo, aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu alipata kura 33 kati ya kura 66 zilizopigwa na wajumbe za nafasi ya ubunge wa viti maalum, wa pili ambaye ni Doris Mushi akipata kura 28 na watatu ni Irene Lema aliyepata kura 4.
Katika mkutano huo, Mbowe aliwashukuru wajumbe wote kwa kumuanini na kumpa nafasi hiyo tena ya kugombea ubunge jimbo la Hai akiwaahidi kuwavusha.
”Nawashukuru wote mlioonyesha imani na mimi kwa kufanya kampeni nzuri na ya kistaarabu na ya kijasiri sana, Mungu awabariki ninyi nyote. Tuendelee kuipigania haki ya kila mmoja wetu,” alisema Mbowe
Leave a comment