Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Maisha ya Rais Mkapa 1938 – 2020
Habari za Siasa

Maisha ya Rais Mkapa 1938 – 2020

Marehemu Rais Benjamin Mkapa akijadiliana jambo na Hayati Julius Nyerere enzi za uhai wao
Spread the love

BABA yake (Benjamin Mkapa) Mzee William Matwani alikuwa mpishi msaidizi katika Mission Ndanda. Wamisionari wakambatiza, wakamfundisha kusoma, kuandika na kuhesabu na kumfanya Katekista.

Alipelekwa Lupaso, ambapo alieneza dini na kufundisha Bush School ya Wamisionari. Alimwoa Bibi Stephania Nambanga ambaye hakujua kusoma wala kuandika. Walijaliwa watoto wanne Benjamin akiwa wa mwisho.

Kama ilivyo kwa kabila la Makua, Benjamin alipewa jina la ujombani, Mkapa. Mama hakuwa na muda wa kujifunza kusoma na kuandika kwani yeye ndiye alikuwa msingi wa familia, akihakikisha analima, kulisha familia na kuwalea watoto.

Ingawa wazazi hawakwenda shule, walipenda sana watoto wao wote waende shule. Hii pamoja na kwamba Baba Matwani alikuwa na kipato kidogo lakini cha uhakika kila mwezi, kiliifanya familia ionekane iko tofauti. Hii ilipelekea wivu na hatimaye chuki kutoka kwa jamii.

Wivu huu na chuki ulisababisha tukio moja baya. Mwaka 1947, kulitokea ukame mkali, basi watu wakamleta mganga wa kienyeji akaamua kuwa mama mzazi, mama yake na bibi yake ndio walikuwa wameloga na kuzuia mvua.

Walipigwa na kuteswa sana hadi Padri Mzungu alipofanikiwa kuwanasua. Bibi wa mama aliaga dunia muda mfupi baada ya tukio hilo. Kijana Benjamini na mwenzie mmoja ndiyo waliopata bahati ya kuendelea na masomo ya sekondari, kutoka darasa la watoto 25 hadi 30.

Shule ya Sekondari ya Ndanda ilikuwa kilometa 60 kutoka Lupaso. Yeye na wenzie walitembea kwa miguu, bila viatu, kwa siku mbili, wakiwa wamebeba kichwani vitu vyao ambavyo vilikuwa vimefungwa katika mkeka. Baadaye alipata sanduku la chuma.

Walimu wa Ndanda walikuwa wamisionari na walikazia sana sala na kazi “Ora et labora’’. Wanafunzi walipika chakula chao wenyewe. Kwa kuwa kijana Benjamini alikuwa mdogo sana, alipewa kazi ya kuosha vyombo.

Kawaida alivibeba vyombo kichwani mpaka mahali pa kuvioshea, na kuvirudisha. Alisema kubeba vyombo hivyo ndiyo sababu ya kuwa na upara. Mwaka 1952, akiwa na umri wa miaka 15, aliamua kwenda Seminari darasa la nane.

Baada ya muda mfupi, aliamua kuwa upadre haukuwa wito wake, akarudi Ndanda kuendelea na shule. Mwaka 1957, alichaguliwa kwenda St. Francis College, Pugu ikiwa ni Shule Kuu ya Wakatoliki Tanganyika.

Akiwa Pugu, kijana Benjamini alianza kupata mwamko wa kisiasa. Aliunga mkono harakati za kupata Uhuru kwa kuandika barua kwa Mhariri wa Gazeti la “Tanganyika Standard” ambalo sasa ni Daily News akiunga mkono hoja ya Uhuru.

Barua ilichapishwa. Ila kijana Benjamini alitumia jina bandia! Mhe. Mkapa alishinda mitihani yake ya kujiunga Chuo Kikuu Makerere, kwa kupata daraja la kwanza, akiwa kati ya wanafunzi watatu bora katika darasa la wanafunzi 51.

Mwamko wake wa kisiasa uliendelea. Alijiunga na Bodi ya Wahariri ya gazeti la “Transition”; alikuwa mwanachama hai wa kikundi cha wanafunzi cha TANU, akiwa katibu na hatimaye mwenyekiti wake.

Alishiriki kwenye siasa za wanafunzi hapo chuoni. Aligombea Urais na ingawa hakushinda, wanafunzi wa kike walimpigia kura nyingi si kwa sababu alikuwa na rafiki wa kike, ila kwa jinsi alivyoweza kujieleza kuliko mpinzani wake.

Aliteuliwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi, na hatimaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi la Wanafunzi hapo Makerere. Alihitimu masomo yake Aprili 1962, miezi minne baada ya Tanganyika kupata Uhuru.

Alipata shahada ya lugha na fasihi ya kiingereza na fonetiki. Alikuwa tayari kuifukuzia nia na ndoto yake.

 Alianza kuajiriwa kama bwana shauri mkufunzi wa Wilaya Aprili 1962. Baada ya miezi mine, August 1962 aliitwa Dar es salaam aende kujifunza udiplomasia Columbia, Marekani.

Baada ya mwaka mmoja alirudi nchini, akaajiriwa wizarani. Kazi yake kubwa ilikuwa kuchukua muhtasari wa mazungumzo ya waziri wake au Rais alipopata wageni.

Siku moja aliambiwa anaitwa Msasani kwa Mwalimu Nyerere. Walipaita Msasani nyumbani kwa Mwalimu “The Clinic”. Mwalimu akamwambia anamteua kuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la The Nationalist.

Mkapa alikuwepo Arusha wakati wa Azimio, mwenzie Nsa Kaisi ndiye aliyebuni neno la Arusha Declaration, walilitumia kwenye The Nationalist, Mwalimu akalipenda, basi hayo maamuzi yakaitwa hivyo.

Mkapa aliruhusiwa kuhudhuria mikutano ya kamati kuu ya TANU, ambayo wakati ule ilitawaliwa na malumbano ya hoja na uchambuzi. Mwalimu na msaidizi wake Joan Wicken ndio walio mfundisha ujamaa.

Aprili 1972 Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Mhariri Mtendaji wa Daily News. Muda mfupi baadaye alimteua kuwa Mwandishi Mkuu wa Rais na juo ndio ulikuwa mwanzo wa maisha yake kama mwanasiasa.

Mwaka huohuo, Mwalimu alimuagiza aanzishe Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) na kuwa Mtendaji Mkuu wake. Mwaka 1976 akamteua Balozi huko Nigeria na mwaka mmoja baadaye akaitwa tena “ The Clinic” na kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje.

Hapa alikuwa kama msaidizi wa Rais kwani Mwalimu ndiye aliyeendesha Mambo ya Nchi za Nje. Alifanywa pia Mbunge wa kuteuliwa. Mwaka 1982 aliteuliwa kuwa Balozi wa Canada na mwaka 1983 hadi 1984 aliteuliwa kuwa Balozi Marekani.

Mwaka 1984 aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje tena.

Baada ya kutafakari na kushauriana na rafiki zake, Mkapa kwanza alimwambia mama Anna Mkapa juu ya kugombea Urais. Mama Anna alisita kidogo ila akakubali.

Pili alimueleza Mwalimu kwa barua kwani alikuwa Butiama, kisha akakutana naye ana kwa ana. Alimpa mwalimu sababu kuu nne za uamuzi wake wa kutaka kugombea.

Alizitaja

  • Kwanza alitaka kurekebisha na kurejesha uhusiano chanya kati ya chama na serikali yake, na vyama vya ushirika ambao ulikuwa umefifia.
  • Pili, alitaka kuhimarisha uhusiano na vyama vya wafanyakazi ambao walikuwa wanatishia kugoma kwa mara ya kwanza.
  • Tatu, ilikuwa kurekebisha mahusiano mabaya na wahisani kuhusiana na kushamiri kwa rushwa.
  • Nne, alitaka kurudisha uhusiano na mashirika ya fedha ya kimataifa ambao walikuwa wamekataa kuanzisha miradi mipya.

November 23, 1995 aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kuunda Baraza la Mawaziri, Mwalimu alikataa kujihusisha.

Kwenye utawala wake alianzisha mifumo na taasisi mbalimbali ili kusaidia kuimarisha uchumi wan chi ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mfumo wa VAT, Public Service and Act, Commision for Human Rights and Good Governance, Takukuru, EWURA, TCCRA, SUMATRA, TANROADS, MKUKUTA, MKURABITA, TASAF.

Kati ya mageuzi aliyofanya yaliyokuwa na utata sana ni kubinafsisha mashirika ya Umma, mageuzi/maboresho ya utumishi, na uuzaji wa nyumba za serikali.

Kuhusu Z’bar

Mkapa anasema, kwenye utawala wake aliingia mashaka pale Rais wa Zanzibar, Salmin Amour alipotaka kubadilisha sheria na kutawala kipindi cha tatu.

Anasema, “lakini baadaye yeye na wafuasi wake wakaamua yaishe.”

Miongoni mwa doa la Mkapa katika utawala wake visiwani Zanzibar ni vifo vya watu 22 vilivyotokea Pemba Januari 2001.

Kwa kauli yake alisema “hili litaendelea kuwa doa katika Urais wangu ingawa sikuwepo lilipotokea.”

Hata hivyo, kwenye utawala wake anasema wanadiplomasia walionesha upendeleo kwa vyama vya upinzani na kukutana nao mara kwa mara.

Kufariki

Marehemu Mkapa amefariki  tarehe 24 Julai, 2020.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!