ASKARI wa Jeshi la Magereza katika gereza la Segerea, wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walikwenda kumsubiri Freeman Mbowe nje ya lango la gereza hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Nguvu hiyo ilitumika baada viongozi na baadhi ya wanachama wa Chadema kufika katika gereza hilo, ili kukamilisha taratibu za kumtoa Mbowe.
Viongozi hao wa Chadema walikwenda Segerea baada ya kukamilisha masharti ya faini ya Sh. 70,000,000, hata hivyo walipofika getini, askari hao waliwazuia kuingia.
Kutokana na kuzuiwa, Halima Mdee, Mbunge wa Kawe na viongozi wengine waliokwenda, walishuka kwenye gari ili kusikilizana na askari hao.
Hivyo, wafuasi wa chama hicho waliokuwa eneo hilo, nao walisogea kusikiliza na kushinikiza viongozi wa Chadema waachwe kwenda kukamilisha taratibu za kumtoa Mbowe.
Askari hao walianza kuwapiga na kukamata baadhi ya wafuasi hao, na walipoona hali inazidi kuchafuka, wakalazimika kutumia mabomu ya machozi jambo lililozua taharuki eneo hilo.
Mmmoja kati ya wafuasi alalamika, kuwa licha ya kukamilisha masharti ya kumtoa Mbowe gerezani, bado mamlaka ya gereza hilo inajizungusha kumtoa.
Leave a comment