Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Huyu ndiye Dk. Hussein Ali Mwinyi
Habari za SiasaTangulizi

Huyu ndiye Dk. Hussein Ali Mwinyi

Dk. Hussein Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Spread the love

WAJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo Ijumaa tarehe 10 Julai 2020, wameonesha kwa kiwango kikubwa jinsi wanavyomuamini Dk. Hussein Ali Mwinyi. Anaandika Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Wamempitisha kuwa mgombea urais visiwani Zanzibar katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2020.

Amepitishwa kwa kupata kura 129 (asilimia 78.65) akifuatiwa na Shamsi Vuai Nahodha aliyepata kura 16 na Dk. Khalid Salum Muhamed aliyepata kura 19.

Dk. Mwinyi aliyezaliwa tarehe 23 Desemba 1966 huko Unguja, Zanzibar, ni mtoto wa Mzee Ali Hassan Mwinyi (Rais wa Pili wa Tanzania).

Dk. Mwinyi anayemaliza muda wake wa kuwatumikia wananchi wa jimbo la Kwahani, Zanzibar lakini bado anatumikia nafasi ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk. Hussein Mwinyi

Katika uchaguzi huo, Dk. Mwinyi atachuana na wagombea wa vyama vingine vya upinzani akiwemo Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo.

Maalim Seif atakuwa anagombea mara ya sita nafasi ya urais tangu alipofanya hivyo kwa mara ya kwanza 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015.

Alivyojitosa kwenye siasa

Dk. Mwinyi alijitosa kwenye siasa mwaka 1999 na mwaka mmoja baadaye 2000, akawania Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani na kushinda.

Alipokuwa mbunge, Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, alikaa katika wadhifa huo hadi mwaka 2005.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Dk. Mwinyi aligombea tena ubunge na safari hii haikuwa Mkuranga bali alirejea nyumbani Jimbo la Kwahani, Zanzibar.

Dk. Mwinyi alichuana na wagombea sita wa vyama vingine lakini kutokana na jimbo hilo kuwa ngome ya CCM, aliibuka mshindi kwa kupata kura 6,239 (asilimia 85.6) akifuatiwa na Mussa Haji Khamis wa CUF aliyeambulia kura 921 (asilimia 12.6).

Kipindi hiko, ilikuwa ni awamu ya kwanza ya Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Dk. Mwinyi aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, alidumu hadi mwaka 2008 alipopelekwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alikokaa hadi mwaka 2010.

Aliporejea tena Kwahani mwaka 2010 kusaka ubunge alishinda ambapo Rais wa wakati huo, Kikwete akamteua kushika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kabla ya kumpeleka Wizara ya Afya tena mwaka 2012 na miezi 19 baadaye (yaani Januari, 2014), akarejeshwa tena Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Baada ya awamu ya Kikwete kuhitimishwa, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Dk. Mwinyi aligombea katika jimbo hilo tena, alishinda.

Historia na uwezo wake ulimsukuma Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano alipoingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015 kumteua katika baraza lake la mawaziri na kumpa nafasi ya Waziri wa Ulinzi.

Dk. Mwinyi ni miongoni mwa waziri wachache wa Rais Magufuli ambao hawajakumbana na ‘kutumbua’ au kuhamishwa wizara tangu alipoteuliwa.

Nini kimemfanya apitishwe?

Mambo yaliyosaidia kumvusha Dk. Mwinyi kizingiti cha mchujo wa wagombea 31 na hatimaye kuteuliwa ni uzoefu wa kutosha, tena wa kuongoza wizara nyeti kabisa.

Tangu mwaka 2001 hadi leo, Dk. Mwinyi ameweza kuhimili vishindo vya uongozi wa wizara tofauti zikiwamo zile nyeti (Ulinzi na Afya).

Mara zote yalipofanywa mabadiliko ya mawaziri wakati wa Mkapa, Dk. Kikwete hata Dk. Magufuli, yeye aliendelea kuwemo.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi akirejesha fomu za kuwania Urais wa Zanzibar ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Kurejeshwa kwake mara kadhaa kwenye Wizara ya Ulinzi kunamfanya aonekane kama mtu anayeijua vizuri nchi hii hivyo anafahamu mambo mengi nyeti tofauti na wanasiasa wengi.

Hata yeye alipozungumza kabla ya upigaji kura kufanyika alisema, endapo watamchagua, atahakikisha ana enzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Dk. Mwinyi alisema, ataendelezas yale yote yaliyoanzishwa na watangulizi wake.

Safari ya elimu

Dk. Mwinyi alianza safari yake ya elimu ya Msingi jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1972 – 1976, Shule ya Msingi Oysterbay, Dar es Salaam.

Kati ya mwaka 1984–1985 wazazi wake walimhamishia Misri na akasoma katika Shule ya Msingi “Manor House Junior” ambako alihitimu elimu ya msingi.

Shule hii ilikuwa na hadhi ya “Middle School za Tanzania” kwa wakati huo. Mwinyi alipelekwa Misri kwa sababu baba yake, Ali Hassan Mwinyi, alikuwa balozi wa Tanzania nchini Misri wakati huo.

Aliporejea Tanzania, alipelekwa Shule ya Sekondari Azania na kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza hadi nne mwaka 1982 – 1984.

Alipohitimu kidato cha nne alipelekwa Shule ya Sekondari Tambaza kusoma kidato cha tano peke yake mwaka 1984 -1985.

Dk. Hussein Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akiwa bungeni

Dk. Mwinyi tangu zamani ni mtu wa kupenda kusaidia watu, aliomba na kuchaguliwa kusomea utabibu wa binadamu. Alianza masomo ya udaktari nchini Uturuki mwaka 1985, kwenye Shule ya Utabibu ya Chuo Kikuu cha Marmara na kuhitimu Shahada ya Utabibu wa Binadamu mwaka 1992.

Kwa sababu hakumaliza kidato cha sita, alipokuwa huko ughaibuni alipitia masomo ya mwaka mmoja ya kujiandaa na udahili wa Chuo Kikuu “Pre University Studies.”

Chuo cha Marmara kinapokea hata wanafunzi wa kidato cha nne kuanza kusomea shahada ya utabibu, lakini lazima wapitie mwaka mmoja wa maandalizi kama alivyofanya Dk. Mwinyi.

Alipohitimu shahada ya kwanza, alirejea Tanzania na kufanya kazi kwa mwaka mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Mwaka 1993, Dk. Mwinyi aliendelea na masomo ya juu ya utabibu kwa kuunganisha.

Safari hii akipelekwa Uingereza katika Hospitali ya Hammersmith ambako alihitimu shahada ya uzamili ya utabibu mwaka 1994 na kuunganisha shahada ya uzamivu ya udaktari hapohapo Hammersmith na kuhitimu mwaka 1997.

Alirejea nchini kwa mara nyingine na kufanya kazi katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Herbert Kairuki (HKMU) kwa miaka miwili hadi mwaka 1999.

Mwaka 2000, Dk. Mwinyi alizidisha nguvu yake ndani ya CCM kwa kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), akashinda na mwaka 2007 aligombea tena NEC na kushinda.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!