Askofu Mkuu TAG ataka kura uchaguzi mkuu zihesabiwa hadharani

Spread the love

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk. Barnabas Mtokambali ameiomba Serikali nchini humo kuhakikisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 uwe huru, haki na amani. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Askofu Mtokambali alitoa ombi hilo jana Ijumaa tarehe 14 Agosti 2020 mbele ya Rais wa Tanzania, John Magufuli katika mkutano mkuu na Baraza Kuu la Kanisa la TAG lililofanyika ukumbi wa Chuo cha Biblia Miyuji jijini Dodoma.

Maaskofu na Wachungaji wa Kanisa hilo kutoka nchi nzima walishiriki.

Askofu Mtokambali alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu cha siku ya uchaguzi kutokuwa siku ya kusali yaani Ijumaa, Jumamosi au Jumapili na sasa uchaguzi utafanyika Jumatano siku ambayo itakuwa ni mapumziko.

Amesema viongozi wa dini wanamatumaini kwamba uchaguzi huo utaendeshwa kwa uhuru, haki na amani.

“Wahenga walisema dalili ya mvua ni mawingu, tumeshaanza kuziona dalili na mvua za uchaguzi huru na wa haki hasa kupitia mchakato wa upatikanaji wa wagombea ndani ya vyama vya vyao vya siasa ambao umeonekana kuwa wa uwazi na wa kidemokrasia,” alisema.

Rais John Magufuli akizungumza na Baraza la Kanisa la TAG

Askofu Mtokambali alisema, “kupitia michakato iliyotumika mgombea aliyeshinda anaonekana na aliyekosa anaonekana waziwazi, hakuna nafasi za hisia zozote za hila wala udanganyifu.”

“Tunaiomba Serikali idumishe uwazi huu pia kwenye uchaguzi mkuu, yaani kuhesabu kura na kutangaza matokeo kufuate utaratibu mzuri uliofanyika kwenye vyama ili kutokea nafasi kwa wale wepesi wa kudhani kila wanaposhindwa wameibiwa kura. Hivyo, kuweka mazingira ya amani na utegamano katika hali ya utete ya nchi,” alisema Askofu Mtokambali.

Anachokizungumza Askofu Mtokambali ni kama kile kilivyokuwa wakati wa kura za maoni za vyama kuwapata wagombea ubunge ambapo michakato ilikuwa wazi ikiwemo kuruhusu baadhi ya mikutano kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari.

Pia, mikutano mikuu ya vyama vya siasa, katika mickakato ya kuwapata wagombea urais na wagombea wenza nayo ilifanyika kwa uwazi na kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari ikiwemo upigaji na uhesabuji wa kura.

Kiongozi huyo wa kiroho, alizungumzia changamoto mbalimbali ambazo bado zinaikabili nchi kuwa, bado kuna changamoto ya mmomonyoko wa maadili hasa kwa vijana, watu kukosa uzalendo, kutoheshimiana, kuvaa mavazi yasiyo na heshima kutothaminia utu wa mtu.

“Vitu kwa upande wa kanisa wanapambana navyo kwa njia ya kuhubiri injiri ya bwana na mwokozi wetu Yesu kristo,” alisema Askofu Mtokambali.

Aliiomba Serikali ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuiongoza nchi wapambane na changamoto hizo ili kuwe na taifa lenye maadili mema, kwani kanisa ambalo halijengwi kwenye maadili mema haliwezi kusimama.

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk. Barnabas Mtokambali ameiomba Serikali nchini humo kuhakikisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 uwe huru, haki na amani. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea). Askofu Mtokambali alitoa ombi hilo jana Ijumaa tarehe 14 Agosti 2020 mbele ya Rais wa Tanzania, John Magufuli katika mkutano mkuu na Baraza Kuu la Kanisa la TAG lililofanyika ukumbi wa Chuo cha Biblia Miyuji jijini Dodoma. Maaskofu na Wachungaji wa Kanisa hilo kutoka nchi nzima walishiriki. Askofu Mtokambali alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu cha siku…

Review Overview

User Rating: Be the first one !

About Danson Kaijage

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!