Friday , 26 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Wafugaji kuku watakiwa kufuata maelekezo ya wataalam
Habari Mchanganyiko

Wafugaji kuku watakiwa kufuata maelekezo ya wataalam

Spread the love

WAFUGAJI wa kuku nchini wameshauriwa kufuata maelekezo ya wataalam na kuongeza uzalishaji ili bei ya kuku kuweza kushuka na jamii kununua na kula vyakula vya lishe kwa kuondokana na magonjwa jambo litakalosaidia Serikali kupunguza gharama kubwa za ununuzi wa dawa za magonjwa ya binadamu ambazo kwa sasa zimefikia kiasi cha Sh. 200 bilioni. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

 Naibu Waziri wa Mifugo na uvuvi, Abdallah Ulega alisema hayo wakati akifunga semina ya mafunzo kwa wajasiliamali na mawakala wa ufugaji wa kuku kutoka mikoa mbalimbali nchini waliokuwa wakipata elimu ya biashara na masoko kutoka kampuni ya kusambaza na kuzalisha kuku aina ya Kroila F1 (AKM).

Waziri Ulega alisema, ulaji wa vyakula vyenye lishe hupunguza bajeti ya dawa za matibabu kwa ajili ya magonjwa mbalimbali kwa binadamu ambapo alisema, Rais Dk. John Magufuli aliingia madarakani mwaka 2015 na kukuta bajeti ya dawa ikiwa ni Sh. 30 bilioni  na sasa amelazimika kuipandisha hadi kufikia Sh. 200 bilioni.

Alisema bado mahitaji ya nyama ya kuku na mayai ni makubwa ikizingatiwa kuwa bado yapo maeneo mengine yenye utapiamlo mkubwa kwa watoto na kwamba kwa kuongeza uzalishaji wa vyakula hivyo itasaidia upatikanaji wake kwa wingi na jamii kupata kwa bei rahisi na kuepukana na kula kuku kwa siku maalum tu.

Alisema Serikali haitapenda kuona inaendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya tiba kwa watanzania na kwamba ifikie wakati watanzania wajenge tabia ya kula lishe wenyewe ili kuepuka magonjwa na fedha hizo ziende kwenye kuimarisha miundombinu na maeneo mengine.

“Leo hii familia nyingi zinakula kuku sikukuu moja kwa nyingine na tena ni X-mas au Idd sasa hapo lishe itapatikanaje, lakini changamoto ya ulaji huo inatokana na uchache wa uzalishaji wake na kupelekea kuku kuwa na gharama kubwa sokoni,” alisema Ulega.

Hata hivyo aliwataka maofisa ugani nchini kuwatambua wafugaji wote wa kuku wa kienyeji na kisasa ili kusaidia Serikali kujua idadi kamili ya kuku waliopo sambamba na kukabiliana na changamoto zinazowakabili wafugaji ili kuongeza uzalishaji kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Waziri huyo alisema utambuzi wa idadi ya wafugaji wa kuku na kuku waliopo nchini utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji hao ikiwemo ukosefu wa masoko, gharama kubwa za dawa, maradhi na gharama kubwa za upatikanaji wa chakula cha kuku.

Ulega alisema, katika kuboresha suala la Tanzania ya viwanda ni muhimu ikafahamika kuwa inatakiwa uwepo wa viwanda vya kuchakata na kusindika ikiwemo vya nyama za kuku kwa ajili kulisha masoko ya ndani na nje ya nchi na kwamba bila kuwa na utaratibu hawataweza kufikia malengo yanayokusudiwa.

Naye Meneja Masoko na Biashara kampuni hiyo ya AKM, Doflian Walt alisema, kampuni hiyo yenye mashamba makubwa matatu nchi za nje ina uwezo wa kuzalisha kuku chotara namba moja kuroila F1 ambao wanauwezo wa kutaga mayai mengi sambamba na kuzaliana kwa wingi.

Alisema tayari wameshatoa mafunzo kwa mawakala wa wafugaji kuku kutoka mikoa ya Mbeya, Dodoma, Arusha na Morogoro lengo likiwa ni kupata wakulima 200 hadi 300 ili waweze kuona ubora wa kuku hao na kuwaingiza kwenye biashaza zao kwa ajili ya kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla.

Naye Mmoja wa mawakala hao, Japhet Itinde kutoka jijini Dar es salaam alisema, nafasi ya ufugaji wa kuku hao aliyoipata anaiona kama ni nafasi pekee ya kumuinua kiuchumi ambapo anawashauri wafugaji kujitokeza kutumia aina hiyo ya kuku katika biashara.

Alisema, mbegu hiyo ya kuku ni nzuri kufuatia kuwa sawa na ya kuku wa kienyeji ambao wana uwezo wa kufugwa mahali popote pale iwe nje au ndani na wakakua bila tatizo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!