Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lipumba maji ya shingo, Maalim Seif kicheko
Habari za SiasaSiasaTangulizi

Lipumba maji ya shingo, Maalim Seif kicheko

Spread the love

KWA mara ya kwanza, Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), amekiri kwamba, chama chake kinahemea pomoni. Anaandika Mwandishi Wetu …(endelea).

Tofauti na awali ambapo, Prof. Lipumba na timu yake walivyojigamba kwamba, kuondoka kwa Maalim Seif Shariff Hamad, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho hakutawatikisa, lakini sasa anakiri wazi myumbo wa chama chake.

Jana tarehe 8 Juni 2019 katika Ofisi Kuu ya CUF iliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam, Prof. Lipumba alisema kuwa, vyama vya upinzani ni mwiba kwa chama chake huku akitaja ACT-Wazalendo ambacho sasa mvumo wake unakuwa siku hadi siku.

Prof. Lipumba akizungumza na viongozi wa chama hicho wa Mkoa wa Dar es Salaam, alitoa kauli iliyoonesha kukiri kauli iliyotolewa hivi karibuni na Maalim Seif alipokuwa kwenye ziara ya kuzindua matawi mawili ya ACT-Wazalenzo, katika Jimbo la Ukonga, jijini humo.

“Wenzetu CUF wakubali tu kwamba, hawana uwezo wa kupambana na ACT-Wazalendo,” alisema Maalim Seif kwenye ziara hiyo akiongeza kuwa “CUF inategemea dola.”

Kuondoka kwa Maalim Seif kwenye chama hicho, kulijibiwa vikali na baadhi ya viongozi waandamizi wa CUF wakieleza kuwa, hawezi kutikisa chama hicho kwa kuwa, ni chama cha wanachama na si mtu mmoja mmoja.

Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu wa CUF bara ambaye alikaimu nafasi ya Maalim Seif, wakati wa mgogoro kati yake (Maalim Seif) na Prof. Lipumba alisema kuwa, kuondoka kwa kiongozi huyo mahiri wa siasa za upinzani visiwani Zanzibar, hatoacha athari yoyote.

Mkutano wa Prof. Lipumba na viongozi wa Dar es Salaam umetoa taswira tofauti na ile ya Sakaya, ambapo amelalamika ACT-Wazalendo kuvunja ngome za chama hicho.

ACT-Wazalendo kimekuwa kikivamia na kuvunja ngome za CUF visiwani Zanzibar, na hata bara jambo ambalo Prof. Lipumba anakiri kukiumiza chama hicho.

Miongoni mwa maeneo ambayo CUF imeathirika kwa kiwango kikubwa dhamaha ya ACT-Wazalendo kwa kukimbiwa na wanachama pia viongozi wake ni Zanzibar, Tanga, Mtwara, Dar es Salaam pamoja na Lindi.

Kutokana na hali hiyo, Prof. Lipumba amatoa wito kwa viongozi hao kukihami chama hicho ambacho kwa maelezo yake, kina maadui wakubwa wawili ambao ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na upinzani hususan ACT-Wazalendo.

CUF imeendelea kuwa mpekwe baada ya kujing’oa kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jambo ambalo limeendelea kupunguza nguvu na ushirikiano kutoka kwenye vyama vingine vya upinzani.

Wakati CUF ikijitenga na vyama vingine vya upinzani, vyama hivyo vimejenga umoja mpya wa vyama vinane, ili kujiongezea nguvu ya kuikabili CCM kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na baadaye mwakani uchaguzi mkuu.

Umoja huo unahusisha Chama Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, Chama cha Umma (Chaumma), NLD, UPDP, CCK, na DP.

Uamuzi wa Maalim Seif kuhamia ACT-Wazalendo, umekipa uhai mkubwa chama hicho ambacho sasa kimekuwa kikifanya kazi ya kupokea wanachama wapya na baadhi ya waliokuwa viongozi wa CUF pia kufungua matawi mapya nchini.

Wiki hii, Mbaraka Chilumba, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana la CUF (JUVICUF) alijiunga rasmi na ACT-Wazalendo akieleza kuwa, baada ya kuondoka Maalim Seif aliyedhaniwa kuwa ndio tatizo, CUF kimepwaya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!