Lissu kupasuliwa kwa mara nyingine

TUNDU Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), muda huu atafanyiwa upasuaji mwingine katika mguu wake wa kulia, ikiwa ni mara ya 20 tangu alipoanza kutibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Lissu amesambaza ujumbe katika mitandao ya kijamii ulioeleza: “Napenda kuwajulisha kwamba ndani ya nusu saa ijayo ninaingia kwenye operesheni nyingine tena.”

Amesema madaktari wamebaini bakteria katika mguu wake wa kulia ambao uliumizwa sana, hivyo wameamua kumfanyia upasuaji ili kuwaondoa.

Operesheni hiyo inayofanyika nchini Ubelgiji ni ya 20 baada ya ile ya 19 ilifanyika mwezi Machi mwaka huu ikiwa ni mwendelezo wa matibabu aliyokuwa akifanyiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikopelekwa akitokea Dodoma baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana.

Lissu amesema baada ya operesheni huo atafanyiwa upasuaji mwingine baadaye wa kuunga mfupa. “Niseme tu naendelea vizuri sana. Ninawashukuru Watanzania kwa kunitibu, kwani wenye jukumu la kufanya hivyo wamekataa lakini Watanzania hawajanitupa.”

Wanamichezo Jumuiya ya Madola ‘wazamia’

WANAMICHEZO nane wa Cameroon hawaonekani katika makazi yao katika michezo ya Jumuiya madola nchini Australia, maafisa wa timu hiyo wamethibitisha. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Afisa wa habari wa timu ya Cameroon, Simon Molombe amesema kutoonekana kwa wanariadha hao wanaamini wametoroka na kwamba wameripotiwa kwa maafisa wa polisi nchini humo.

Amesema wanyanyua vyuma vya uzito watatu na mabondia watano walionekana mara ya mwisho katika muda tofuati Jumatatu na Juamnne.

Cameroon imesema kundi la wanariadha hao wana viza halali za kudumu hadi Mei 15.

Wanamichezo waliotoweka kambini ni pamoja na Olivier Matam Matam, Arcangeline Fouodji Sonkbou na Petit Minkoumba, wanaonyanyua vyuma vya uzito na mabondia Christian Ndzie Tsoye, Simplice Fotsala, Arsene Fokou, Ulrich Yombo na Christelle Ndiang.

Serikali ya Australia imewaonya wanariadha dhidi ya kukaa zaidi ya muda walioruhusiwa.

Shirikisho la michezo hiyo ya Jumuiya ya madola limesema litaikagua hali hiyo, lakini limeongeza kwamba wanariadha wana “haki ya kusafiri kwa uhuru” kwa viza walizo nazo.

Polisi ya Australia imejulishwa kuhusu hali inavyoendelea, kwa mujibu wa Kate Jones, waziri katika jimbo la Queensland.

Mch. Msigwa aweka rehani ubunge wake kisa Makonda

MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema yupo tayari kujiuzuru ubunge wake kama itathibitika kuwa amemtelekeza mtoto kwa mwanamke mmoja jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwanadishi Wetu … (endelea).

Mch. Msigwa ametajwa na mwanamke mmoja kati ya walioripoti katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa ametelekeza mtoto.

Makonda ametoa nafasi kwa wanawake waliotelekezwa na wanaume waliowazalisha, ndipo mwanamke huyo ambaye hajatajwa jina lake alifika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa na kueleza kuwa amezalishwa na mbunge huyo na kumtelekeza bila matunzo yoyote.

Katika taarifa yake, Mch. Msigwa amesema kinachoelezwa kuwa ametelekeza mtoto jijini na mwanamke huyo ni propaganda za makusudi zenye lengo la kujaribu kumchafua.

Msigwa amesema: “Kama huyo mama ambaye jina lake limehifadhiwa yupo, nataka ajitokeze pamoja na mtoto niliyemtelekeza. Kwa sasa nipo Dodoma Bungeni; anaweza kunipata kupitia Spika wa Bunge au Katibu wa Bunge au Kiongozi wa Upinzani Bungeni.”

Mbunge huyo amesema kama ikithibitika kuna mtoto amemtelekeza yupo tayari kujiuzuru Ubunge.