Rais Magufuli amtumbua Mkurugenzi

RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa, Mohamed Maje kuanzia leo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Akitoa taarifa ya utenguzi huo mjini Dodoma, Katibu Mkuu wa Tamisemi, Alhaji Mussa Iyombe amesema kuwa Maje ameisababishia serikali hasara ikiwemo kushindwa hata kukusanya mapato ya serikali.

Utenguzi wa Maje umetokana na taarifa iliyotolewa na tume iliyoundwa kukagua utendaji wake wa kazi nakubaini kuwa ameshindwa kusimamia na kudhibiti mapato ya halmashauri hali iliyopelekea upotevu wa fedha.

“Hadi kufikia robo tatu ya mwaka wa fedha halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa imekusanya mapato kwa asilimia 24 tu pamoja nakuwa halmashauri hiyo ni kongwe na yenye vyanzo vingi vya mapato,” amesema Iyombe.

Hatua hii imekuja baada ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk. Bilineth Mahenge kuagiza kuundwa kwa tume ya mkoa kuchunguza ubadhilifu wa fedha zaidi ya Sh. 500 milioni katika halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa pamoja na kubaini sababu za halmashauri hiyo kuwa ya mwisho katika ukusanyaji wa mapato.

Akizungumza katika kikao cha ushauri wa mkoa (RCC) Mahenge alionyesha kusikitishwa na matokeo hayo pamoja na kuwa wilaya Kongwe nayenye vyanzo vingi vya mapato kukusanya asilimia 24 pekee ya mapato hivyo kupelekea kuchukuliwa hatua kwa watendaji wote wanaokwamisha ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Hata hivyo Mahenge alisisitiza uadilifu kwa watendaji ikiwa ni pamoja na kupeleka mashine za kukusanyia mapato katika kata.

“Ukusanyaji wa mapato ya ndani ni muhimu sana katika halmashauri kwani ndio hutumika katika shughuli za maendeleo,ukuaji na ustawi wa halmashauri,” amesema Mahenge.

Wambura ashindwa rufaa, sasa kuburuzwa mahakamani

KAMATI ya Rufaa za Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetupilia mbali rufaa ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura, hivyo adhabu aliyopewa na Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo itaendelea. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Wambura alifungiwa kutojihusisha na kujishughulisha na masuala ya mpira wa miguu maisha yake yote na Kamati ya Maadili ya TFF kwa makosa matatu ikiwemo la kupokea au kuchukua fedha za shirikisho hilo kwa malipo ambayo hayakuwa halali.

Akisoma hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa za Maadili ya TFF, Ebenezer Mshana amesema wamesikiliza pande zote mbili za mrufani na mjibu rufani na kuzitupilia mbali rufaa zote za Wambura kutokana na kutokuwa na hoja za msingi.

Mshana amesema rufaa ya Wambura iliyopelekwa mbele ya kamati yao haina mashiko hivyo wameridhia adhabu aliyopewa katika Kamati ya Maadili kama ilivyoamuliwa ya kufungiwa maisha kujihusisha na soka.

Pia Mshana ameshauri TFF kupeleka tuhuma zilizomtia hatiani Wambura zipelekwe katika vyombo husika ili hatua nyingine zaidi zichukuliwe.

Mshana amesema mawakili wa mrufani walijikita zaidi katika hoja za mteja wao kutopewa nafasi ya kusikilizwa lakini hawakuwa na hoja hata moja ya kupinga mashtaka yaliyomtia hatiani katika Kamati ya Maadili.

Makosa mengine yaliyomtia hatiani Wambura mbali na kuchukua fedha za TFF, ni kugushi barua alipwe fedha za kampuni ya Jeck System na kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho hilo.

 

Shule, Vyuo binafsi walalamikiwa rushwa ya ngono

SERIKALI imesema kuwa baadhi ya Mameneja, Wakurugenzi pamoja na wamiliki wa shule binafsi na vyuo wanalalamikiwa kwa vitendo vya rushwa ya ngono hasa wakati wa kutoa ajira kwa walimu hususani jinsia ya kike. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Elimu, Joseph Kakunda alipokuwa akifunga mkutano wa Shilikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali (TAMONGSCO) uliofanyika kitaifa mjini hapa.

Kakunda amesema kwamba licha ya kuwa shule za binafsi pamoja na vyuo vinamchango mkubwa katika jamii pamoja na serikali kuzitambua lakini yapo maeneo yanayolalamikiwa ikiwa ni pamoja na masuala ya rushwa.

“Yapo maeneo ya rushwa hasa katika rushwa ya ngono ni jambo la aibu hata hivyo wanaume wengi ndio wanaoongoza kuomba rushwa ya ngono,wanawake wengi wa Afrika hasa wa Kitanzania wanajiheshimu sana hivyo wanaume igeni mfano wa wanawake wengi.

“Rushwa ya ngono imekuwa ikilalamikiwa hasa wakati wa kipindi cha uombaji wa ajira najua siyo shule zote wala vyuo vyote vya binasi lakini kwa baadhi ya wanaofanya hivyo wanatakiwa kuacha mara moja kwani ni aibu kuwepo kwa vitendo hivyo,” amesema Kakunda.

Akizungumzia kuwepo kwa shule binafsi Kakunda amesema kuwa wapo baadhi ya Mameneja na Wamiliki ambao wanaendesha shule hizo kama biashara kwa kutoza ada kubwa na kusababisha hata wale waliopakana na shule hizo kushindwa kujiunga na shule hizo kutokana na kiwango kikubwa cha ada.

Kutokana na hali hiyo amewataka mameneja na wamiliki kurudi katika mwongozo wa sera ya elimu na mazingira ya usawa na uwezeshaji na isiwe katika misingi ya kibiashara.

“Zipo shule zenye majina makubwa kalini watoto wa jirani na shule hizo hawasomi hapo, hata mameneja na wamiliki hawatembelei wazazi na kuwaelezea mikakati ya shule zao na bei za ada wanazotoza hata kuwashawishi kuwa wanaweza kutoa ada kwa awamu ngapi ili kuwashawishi wazazi hao kuwa na mwamko wa kusomesha watoto katika shule hizo,” amesema Kakunda.

Katika hatua nyngine hakusita kuzungumzia baadhi ya shule binafsi kushindwa kutoa mikataba ya ajira kwa watumishi wao ikiwa ni hatua moja wapo ya kutowaingiza katika mifuko ya jamii watumishi hao jambo ambalo amesema ni ukiukwaji wa misingi ya utoaji wa ajira.

Amesema kutokana na hatua hiyo serikali haitasita kuwachukulia hatua wamiliki na mameneja watote ambao watakiuka utoaji wa mikataba kwa watumishi wao ikiwa ni pamoja na kutowapa fursa ya kujiunga katika mifuko ya kijamii.

Kakunda pia amekemea baadhi ya shule pamoja na vyuo binafsi ambavyo vinajiendesha bila kuwa na bodi ikiwa ni pamoja ya kuwafukuza wanafunzi bila kufuata utaratibu alisema kuwa pia zipo ambazo hazifuhati mihura rasmi ya serikali jambo ambalo kiongozi huyo alisema kuwa halikubaliki.