May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zuio NGOs kuishtaki Serikali Afrika: Samia aonesha matumaini

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema atalifanyia kazi ombi la kuitaka Tanzania ibadili msimamo wake, wa kujitoa kwenye azimio linaloruhusu Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) na watu binafsi , kuishtaki Serikali kwenye Mahakama ya Haki za Binadamu na Watu Afrika. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi tarehe 27 Mei 2021, akizungumza na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, anayemaliza muda wake, Sylvain Ore, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mwishoni mwa 2019, chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, Tanzania iliamua kuitoa itifaki inayowaruhusu wananchi na NGOs kuishtaki Serikali katika mahakama hiyo, kwa maelezo kwamba inapingana na sheria za nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Samia amesema, wakati Serikali yake inaliangalia suala hilo, zuio hilo litaendelea kutekelezwa kama kawaida.

“Kuhusu Tanzania kufuta tamko la kuruhusu taasisi zisizo za kiserikali na watu binafsi, kupeleka mashauri yao moja kwa moja katika mahakama hiyo. Rais Samia amesema Tanzania italiangalia jambo hilo, lakini kwa sasa msimamo haujabadilika,” imesema taarifa ya Msigwa.

Kwa upande wake Ore, amesema mahakama hiyo itaendeleza ushirikiano na Serikali ya Rais Samia.

“ Ore amemshukuru Rais Samia kwa ushirikiano ambao mahakama hiyo imeupata, kwa kipindi chote cha uongozi wake na amemhakikishia kuwa Tanzania ni sehemu sahihi ya mahakama hiyo,” imesema taarifa ya Msigwa.

error: Content is protected !!