September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Mkuu kufungua mkutano wa walinzi

Spread the love

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kufungua mkutano mkuu wa kazi wa chama cha sekta binafsi ya Ulinzi nchini (TSIA) leo jijini Dodoma unaolenga kujadili changamoto zinazokabili sekta hiyo. Anaripoti Danson Tibason, Dodoma … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa Mkurugenzi mtendaji wa chama hicho Isaya Maiseli, alisema kuwa mkutano huo ni wa kazi ambao utatumika kutathimi changamoto na mafanikio kwa mwaka 2018.

Alisema mkutano huo pamoja na kujadili changamoto na mafanikio pia utatumika katika kuweka mikakati ya utendaji kazi kwa mwaka 2019.

“Pamoja na kujadili changamoto na mafanikio tuliyoyapata katika mwaka ulioisha pia tutajadiliana mambo mbalimbali ambayo yamekuwa changamoto kwetu toka tumeanzisha chama chetu kwa zaidi ya miaka 38 sasa,”alisema Maiseli.

Aidha alisema kuwa katika mkutano huo wataalika maofisa kutoka jeshi la polisi ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kipindi kirefu.

Hata hivyo alitaja moja ya changamoto zinazowakabili kuwa ni kutokuwepo kwa sheria ambayo inawatambua wao hali inayosababisha kufanya kazi chini ya miongozo ya jeshi la polisi.

Alisema pamoja na kuendelea kuiomba serikali kuweka sheria ambayo ingeweza kuweka mazingira rafiki katika utendaji kazi wao imekuwa ikipiga danadana kwa muda wote huo.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa vitendea kazi katika makampuni yao ya ulinzi hali ambayo inasababisha wafanyakazi kufanya kazi katika mazingira magumu

“Pia wateja wengi  wanaohitaji huduma hii ya ulinzi wamekuwa wakitaka watu wa bei nafuu hali ambayo inasababisha makampuni mengi kushindwa gharama za kujiendesha,”alisema.

Naye, Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Dodoma Lucanusi Kayombo, alisema kuwa wao kama wenyeji wa mkutano huo wamejiandaa katika kufanikisha mkutano huo kwa ufanisi mkubwa.

error: Content is protected !!