Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imefanikiwa kutoa jumla ya mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 28 kwa wateja zaidi 20,000 katika maeneo mbalimbali hapa nchini kupitia huduma yake maalum kwa wateja wa Kiislamu inayojulikana kama La Riba, ambayo inazingatia mafundisho ya Kiislamu kuhusu riba. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Hayo yamebainishwa jana Ijumaa jijini Dodoma katika hafla ya futari mahususi kwa wateja wake wa Kiislamu iliyoandaliwa na benki hiyo.
Hafla hiyo iliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Senga Gugu aliyemuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Hamad Masauni.
Mkurugenzi wa Mikopo wa NBC, Salehe Mohammed alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi kwenye hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na wageni mbalimbali waalikwa wakiwemo wateja na viongozi waandamizi serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri aliemuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Rosemary Senyamule pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Gerald Mongela.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Salehe alisema kumekuwa na muitikio mzuri kutoka kwa wateja kuhusiana na huduma ya La Riba inayozingatia misingi ya dini ya Kiislamu katika masuala ya riba.
“Zaidi tunajivunia kuona kwamba huduma hii imejipambanua kama msaada mkubwa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wenye imani ya dini ya kiisalamu. Tumekuwa tukitumia vema hafla kama hizi kuitangaza huduma hii muhimu na matunda ya jitihada zetu yanazidi kuonekana,’’ alibainisha Mohammed.
Akizungumzia hafla hizo, Mohammed alisema ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuandaa hafla za namna hiyo maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kipindi cha miaka 15 mfululizo hadi sasa ikilenga kuonyesha mshikamano na umoja katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Katika hotuba yake, kwenye hafla hiyo hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Senga Gugu aliipongeza benki ya NBC kwa ushirikiano wake na wadau wake huku akisisitiza umuhimu wa huduma bora za kifedha zinazoheshimu imani za kidini katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa sambamba na kuleta utulivu na amani ya nchi.
Hafla hiyo pia ilitoa fursa kwa wateja hao kufurahi pamoja na kujenga uhusiano mzuri miongoni mwao na benki hiyo.
Leave a comment