IMEELEZWA kuwa ushirikiano, ubunifu, mbinu za kisasa kwenye usimamizi wa sekta ya nishati nchini utafanikisha sekta hiyo kuwa endelevu na salama. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx nchini, Kalpesh Mehta akichangia mjadala kwenye Kongamano la Nishati Tanzania linafanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIC), jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo alisema sekta ya nishati ni kubwa na muhimu kwa maendeleo, jamii na uchumi wa nchi na watu wake hivyo njia ya kufanikisha sekta hiyo ni kuwekeza katika kila eneo.
Mehta alisema matamanio ya Tanzania ni makubwa kupitia sekta hiyo, hivyo njia ya kukidhi matamanio hayo ni kuwepo na mazingira rafiki na endelevu.
Alisema sekta hiyo ni muhimu katika maendeleo ya nchi, hivyo uendelevu wake unakuwepo kwa wahusika na sekta hiyo kutumia vipawa vyao, mbinu za kisasa na ushirikiano.
Mehta alisema hitaji la dunia ni kuona matumizi ya nishati safi, salama na endelevu yanaongezeka, hivyo kinachohitajika ni waliopo katika sekta hiyo kuwa sehemu ya mabadiliko.
“Ajenda kuu ya dunia ni kuona namna gani nishati jadidifu inapewa kipaumbele, hivyo ni vema watu wote wenye vipawa na wabunifu kuonesha uwezo wao kuhakikisha sekta hiyo inapiga hatua chanya,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema iwapo wadau wote kuanzia Serikali, sekta binafsi na watumiaji wa rasilimali zinatokana na nishati watakuwa kitu kimoja ni wazi sekta hiyo itakuwa endelevu.
Mehta alisema ni vema msukumo ukaongezeka katika uwekezaji kwenye maeneo ambayo yataweza kuzalisha nishati ambayo ni safi na salama.
Mkurugenzi huyo wa Oryx alisema changamoto ya watu wenye kukidhi soko la ajira kwenye eneo hilo ni kubwa, hivyo juhudi zinahitajika ili kuziba pengo hilo.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzan Ndomba alisema taasisi yao imekuwa ikishirikiana na waajiri kuhakikisha mazingira rafiki ya kutekeleza miradi yenye mwelekeo wa nishati safi na salama.
Alisema juhudi zao zimejikita katika kuhakikisha elimu inatolewa, ikiwemo na kuweka msukumo wa kupata mitaala yenye kukidhi soko la ajira.
Leave a comment