VIONGOZI wa vituo vya huduma za afya vya umma, wametakiwa kuchukua tahadhari ya matumizi ya fedha kulingana na bajeti ya serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Kauli hiyo imetolewa na Dk. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 21 wa kutathimini utekelezaji wa vipaumbele vya kisera katika sekta ya afya uliofanyika jijini Dodoma leo tarehe 22 Disemba 2020.
Dk. Gwajima amesema, bado kuna malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu ukosefu wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini .
“Ili kufikia azma ya rais, sisi kama sekta ya afya inabidi kuongeza kasi katika uwajibikaji wa pamoja katika malengo tuliyoyaweka.
“Ni lazima tufanye upekuzi wa matumizi ya fedha za dawa, vifaa na maabara lazima ziheshimike na kufika kwa mgonjwa ili wananchi watuamini na kuweza kutatua kero zao,” amesema.
Amesema, katika kutekeleza hilo, wizara itatoa maelekezo ya kuongeza ufanisi katika uwajibikaji kuanzia kwa watumishi wote wa sekta ya afya, ngazi mbalimbali za usimamizi na uendeshaji.
Kuhusu tiba asili na tiba mbadala, Dk. Gwajima amesema zimekuwa zikisaidia katika kutibu magonjwa mbalimbali kwa wananchi na hivyo serikali inakusudia kuimarisha kitengo cha utafiti wa tiba mbadala.
Dk. Festo Dugange, Naibu Waziri Ofisi ya Rais -TAMISEMI amesema, ili kufikia lengo la kuwawezesha wananchi wote kuwa na bima ya afya, kunahitajika kuimarisha mifuko ya bima hiyo ili kuwafikia wananchi wengi.
“Mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa kwa sasa unachangia asilimia tano ya wanufaika wote waliojiunga katika mifuko ya bima za afya nchini.
“Katika kipindi cha utekelezaji wa mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa kuanzia Julai 2018, tumefanikiwa kusajili kaya 557,882 sawa na wanufaika 3,347,112 kufikia Novemba 2020,” amesema Dk. Dugange.
Leave a comment