Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa TRA yashindwa kukusanya Sh. 712 bilioni
Habari za Siasa

TRA yashindwa kukusanya Sh. 712 bilioni

Spread the love

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) nchini Tanzania, imebaini hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2020 zaidi ya Sh. 712.4  bilioni hazikukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma leo Ijumaa tarehe 22 Mei 2020, na Aeshi Hilaly, Makamu Mwenyekiti wa PAC, TRA imeshindwa kukusanya kiasi cha Sh. 712.4 bilioni, kutokana na dosari mbalimbali katika Idara ya Ushuru na Forodha.

Taarifa ya PAC inaeleza, kiwango hicho cha fedha hakijakusanywa hadi mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2019.

“Changamoto kubwa katika idara ya ushuru na forodha ni suala la ufuatiliaji wa karibu wa taratibu za forodha pamoja na kutofanyika usuluhishi (Tax reconciliation) wa makusanyo ya kodi kwa wakati,” amesema Hilaly

Hilaly amesema, PAC imebainisha mapato ambayo hayajakusanywa kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo, mapato ya kiasi cha Sh. 127. 88 bilioni ya bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi, ambazo hazikuwa na uthibitisho wa kutoka nchini Tanzania.

“Mafuta yaliyoagizwa kutumika hapa nchini bila kuwa na uthibitisho wa malipo ya kodi na riba kiasi cha Sh. 265.28 bilioni. Na kiasi cha  Sh. 88.55 milioni za bidhaa zilizoagizwa na kupatikana kuwa na dosari katika mchakato wa forodha,” amesema

Mapato mengine ambayo hayajakusanywa  na TRA ni  Sh. 2.25 bilioni za bidhaa zilizoagizwa kwa matumizi ya muda hapa nchini,  lakini zimekosa uthibitisho wa kusafirishwa nje ya nchi.

Wakati huo huo, PAC  imebaini kwamba, hadi kufikia tarehe 30 Juni 2019, jumla ya mashauri ya kodi Sh. 84.6 bilioni, yalikuwa hayajahitimishwa kwa wakati.

“Hali hii kwa kiasi kikubwa inachangiwa na vyombo vinavyohusika na utoaji wa maamuzi ya kodi, Bodi ya Rufaa ya Kodi ( TRAB) na Baraza la Rufaa za Kodi ( TRAT), kutotekeleza majukumu yake ya kisheria kwa wakati, kutokana na sababu mbalimbali,” inaeleza taarifa ya PAC.

Halikadhalika, PAC imebaini TRA ilishindwa kukusanya madeni ya kodi za siku za nyuma, zaidi ya  Sh. 303 bilioni.

“Kwa upande wa changamoto ya ukusanyaji wa madeni ya kodi za siku za nyuma (Tax arrears), hadi kufikia tarehe 20 Aprili, 2020, jumla ya deni la kodi la kiasi cha shilingi 303,091,352,906, lilikuwa bado halijakusanywa na TRA,” inaeleza taarifa ya PAC.

Kufuatia changamoto hiyo, PAC imeishauri Serikali iiwezeshe TRA katika kushughulikia mashauri ya kikodi na ukusanyaji wa madeni ya kodi.

“Serikali iimarishe mifumo ya udhibiti katika huduma za utoaji mizigo na ulipaji wa kodi kwa bidhaa zinazoingizwa ndani ya nchi, kwa kuhakikisha huduma zote za forodha zinafuatwa ipasavyo, ili kuepuka upotevu wa mapato ya Serikali,” imeshauri PAC

“Mwisho, Serikali iimarishe udhibiti na ufuatiliaji wa mizigo inayopitia hapa nchini kwenda nje ya nchi (Transit goods), ili kuepuka matumizi ya bidhaa hizo katika soko la ndani bila ya kulipiwa kodi.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!