July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

THRDC yataka tume huru uchunguzi sakata la Loliondo

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Spread the love

 

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umeiomba Serikali ihakikishe maridhiano yanapatikana katika utatuzi wa sakata la Loliondo, kwa kuunda tume huru kwa ajili ya kuchunguza wamasai waliokimbilia Kenya, pamoja na kuwaacha huru viongozi iliyodai wamebambikiwa kesi ya mauaji ya askari. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Maombi hayo yametolewa leo Alhamisi, tarehe 23 Juni 2022 na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, akizungumzia kikao cha wadau wa haki za binadamu na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kujadili namna ya kuimarisha haki za binadamu, katika mchakato wa uwekaji alama za mipaka kwenye Pori Tengefu la Loliondo na uhamishaji kwa hiari wananchi wa Tarafa ya Loliondo.

Olengurumwa ameiomba Serikali iunde tume ya uchunguzi ili kubaini kama wamasai waliokiimbilia Kenya kwa sababu mbalimbali ikiwemo za matibabu baada ya kujeruhiwa kutokana na sakata hilo, ni Watanzania kwa ajili ya kuwarudisha nchini.

Wito huo umetolewa baada ya kuibuka tuhuma ya kwamba wamasai waliokwenda kutibiwa Kenya sio Watanzania, wakati Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Oleshangai, akidai ni wananchi wake na kwamba wamekwenda kutibiwa nchini humo baada ya kukosa fomu ya Polisi namba tatu (PF3), inayotolewa kwa raia aliyepata majeraha.

“Kuhusu watu walioenda Kenya tumeshauri kuwe na timu ya pamoja itakayohusisha watetezi wa haki za binadamu, waende Kenya kubainisha Watanzania ili warudishwe bila masharti yoyote. Hii itasaidia kuondoa aibu kama Taifa kimataifa na kurudisha imani ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wake,” amesema Olengurumwa.

Katika hatua nyingine, Olengurumwa ameiangukia Serikali akiiomba ifanye uchunguzi wa kina ili kubaini kama viongozi wa wananchi ikiwemo madiwani wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya Askari Polisi, walihusika na tukio hilo na kama hawajahusika waachwe huru na aliyehusika achukuliwe hatua.

“Tunafahamu wale wenzetu wako ndani ni viongozi 10, wakiwemo madiwani sita na wa viti maalum wanne. Tunaamini kesi imeenda harakaharaka wako wameingia kimakosa. Tunaishauri Serikali uchunguzi ufanyike haraka kubaini waliohusika na mauaji ili aliyempiga askari kwa mshale apatikane sheria ichukue mkondo wake na si kuwaingiza wengine,” amesema Olengurumwa.

Hata hivyo, Olengurumwa amesema watetezi wa haki za binadamu wanalaani tukio la mauaji hayo, na kuwataka wananchi wa Ngorongoro kufuata njia stahiki katika kudai haki yao badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Katika hatua nyingine, Olengurumwa ameliomba Bunge litende haki wakati linapojadili sakata hilo lililotokana na mgogoro wa ardhi kufuatia ongezeko la idadi ya watu, makazi na mifugo, badala ya kuegemea upande mmoja.

“Bunge lisiwe na upande wowote, yale maneno yanayoleta upendeleo yasiwepo bungeni,” amesema Olengurumwa.

error: Content is protected !!