Tuesday , 21 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa TARURA yashauriwa kuacha ujenzi wa barabara za uzito wa tani 10
Habari za Siasa

TARURA yashauriwa kuacha ujenzi wa barabara za uzito wa tani 10

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dk. Festo Dugange
Spread the love

 

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wametakiwa kuachana na ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zenye uwezo wa kubeba magari yenye uzito wa tani 10 na badala yake wajenge barabara zenye uwezo wa kuhimili uzito wa tani 30 ili kuongeza tija kwa wananchi katikika shughuli za usafirishaji wa mazao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI), Abdallah Chaurembo wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Mkoa wa Iringa kukagua ujenzi wa barabara za mradi wa “Agri-Connect” unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jumuia ya Ulaya katika wilaya za Mufindi na kilolo.

“Tumeona barabara hii imejengwa kwa uwezo wa kupitisha tani 10, sisi kamati tumeshauri TARURA wajenge barabara zenye uwezo wa kuhimili tani 30 ili wananchi wafanye biashara zao za mazao kwa furaha bila bughudha,” alisema Chaurembo.

Pia alieleza kuwa wananchi kwa muda mrefu walikuwa na kilio cha barabara ambazo zinatoka kwenye uzalishaji kupeleka masokoni, ambapo mradi huu sasa umejibu kilio hicho baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia fedha za ujenzi kwa barabara hizo ambazo sasa zimerahisisha usafirishaji.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya) Dk. Festo Dugange alisema kazi kubwa na nzuri imefanyika katika ujenzi wa barabara hiyo ambayo itafungua uchumi na kurahisisha shughuli za kijamii kwa wananchi.

“Dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia ni kuhakikisha kuwa inafungua miundombinu na uchumi wa wananchi wakiwemo wananchi wa Mufindi. Hivyo, tunatarajia barabara hii sasa itakuwa mkombozi mkubwa wa kiuchumi na shughuli za kijamii; na jukumu la OR-TAMISEMI ni kuhakikisha kwamba barabara zinajengwa kwa ubora na kukamilika kwa wakati na kutimiza malengo ya Serikali yaliyopangwa, “alisema Dk. Dugange.

Naye mjumbe wa kamati hiyo, Thea Ntara alisema barabara hiyo itawasaidia wakulima siyo tu wa mazao ya chai na mbogamboga bali hata wakulima wa mazao ya miti kama mbao na magogo hivyo kusaidia kukua kwa uchumi wa wananchi wa Mufindi na mkoa wa Iringa kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kuwavutia wawekezaji.

Kwa upande mwinginne Diwani wa kata ya Mtwango, Monte Kalamlya alisema barabara hiyo imekuwa ni chachu kwa wananchi wa kata ya Luhunga na wanaotoka vijiji vya jirani kwa sababu imefanya nauli zimepungua na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao ambalo ni lengo la serikali kuhakikisha kuwa maisha ya mwananchi yanakuwa nafuu.

“Kwakweli kupitia barabara hii mazao yetu ya chai yatafika haraka kwenda kiwandani na uchumi sasa utaenda kufunguka kwa kasi na maendeleo yatapatikana, na wananchi wameipokea kwa mikono miwili,” alisema Mtwango.

Mradi wa Agri-Connect katika Mkoa wa IIringa, wilaya ya Mufindi unahusisha barabara ya Sawala- Mkonge-Iyegeya yenye urefu wa kilomita 30.3 iliyojengwa kwa thamani ya shilingi 8,167,087,887.00.

Mradi huo lengo lake kuu ni kurahisisha usafirishaji wa mazao ya Mboga mboga, Chai, matunda na mazao mengine toka mashambani kwenda mikoa mingine au kwenda viwandani ama katika maghala ya kuhifadhia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Watumishi 25,039, taasisi 65 wahamia Dodoma

Spread the loveSerikali imesema hadi sasa, jumla ya watumishi 25,039 kutoka Serikali...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Balozi Nchimbi aonya maofisa utumishi kuacha uonevu

Spread the loveKatibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Balozi Kasike ateta na mjumbe wa FRELIMO

Spread the loveBalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji, Phaustine...

Habari za SiasaKimataifa

Kiongozi Mkuu Iran amteua mrithi wa Rais Ebrahim

Spread the loveKiongozi wa ngazi ya juu nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei,...

error: Content is protected !!