RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameonesha kusikitishwa na mifarakano inayotokea katika nyumba za ibada baina ya viongozi wa dini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).
“Mnakuwa na mifarakano watu wanagombana wanafika kuchukuliana hatua kubwa,” amesema Rais Samia leo Ijumaa tarehe 10 Juni, 2022 ikiwa ni siku chache tu tangu viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde kufikishana Mahakamani kutokana na migogoro baina yao.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa msikiti uliojengwa na Jumuiya ya Istiqaama mjini Bukoba mkoani Kagera, Rais Samia amesema katika maeneo mengine inazuka mifarakano misikiti inapojengwa hasa ikiwa na vitega uchumi.
Amesema mifarakano inatokea katika kutaka madaraka ya kusimamia na kuendesha misikiti, “hasa kunapokuwa na vibiashara vya kuleta riziki kwenye msikiti huo.”
“Si matumaini yetu kusikia kuna mifarakano kwenye nyumba za ibada, kwenye nyumba za kuabudu Mungu, mnakuwa na mifarakano watu wanagombana wanafika kuchukuliana hatua kubwa, si matumaini yetu kuona mnaelekea huko,” amesema Rais Samia.
Leave a comment