October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais wa wanafunzi Ruaha afikishwa kortini tuhuma za wizi

Spread the love

CHRISTOPHER Michael Mollel, aliyekuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha (CDTI), anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani Iringa kwa makosa manne ikiwemo wizi wa Sh. 1.25 milioni. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Makosa mengine yanayomkabili Mollel ni, kughushi nyaraka kinyume cha sheria, kuwasilisha maelezo ya uongo na kutoa taarifa ya uongo kwa mtu aliyeajiriwa katika mamlaka ya umma.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu tarehe 29 Juni 2020 na Mweli Evart Kilimali, Mkuu wa Takukuru mkoani Iringa.

Kilimali amesema, mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda makosa hayo tarehe 25 Okoba 2020 akiwa rais wa wanafunzi wa chuo hicho, ambapo alighushi nyaraka na kutoa taarifa za uongo ili kuiba Sh. 1.25 milioni fedha ambazo zilikuwa za taasisi ya wanafunzi wa CDTI.

“Uchunguzi wa Takukuru mkoa wa Iringa ulibaini tarehe 25 Oktoba 2019, mtuhumiwa akiwa ndiye rais alichana na kuiba hundi namba 000063 kutoka katika kitabu cha hundi Cha Ruaha CDTI Student Organization, kilichokuwa kimehifadhiwa ofisini kwa mshauri wa wanafunzi wa chuo hicho,” amesema Kilimali.

Kilimali amesema, baada ya mtuhumiwa huyo kuiba hundi hiyo, aliijaza taarifa za uongo za kutakiwa kulipwa fedha kiasi cha 1.25 milioni ambapo alisaini kama mmoja wa watia saini katika kaunti hiyo, na kughushi saini ya mtia saini wa pili katika akaunti hiyo.

“Pia, uchunguzi umebaini tarehe 26 Oktoba 2019, aliiwasilisha hundi hiyo namba 000063 ya akaunti namba 60510007147, katika benki ya NMB akiwa ameambatanisha na nakala ya kuwekea hundi ambayo ilikuwa na maelekezo ya kutoa fedha kiasi cha 1,250,000, kutoka katika akaunti ya taasisi hiyo,” amesema Kilimali.

Kilimali amesema, uchunguzi wa makosa hayo umekamilika na kwamba Mollel amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa, kujibu tuhuma zake.

“Uchunguzi umekamilika na Takukuru Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, inatarajia kumfikisha mtuhumiwa mahakamani leo tarehe 29 2020 katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa,” amesema Kilimali.

error: Content is protected !!