Saturday , 4 May 2024
Home Habari Mchanganyiko MSCL kujenga meli ya mizigo, abiria kwenda visiwa vya Comoro na Shelisheli
Habari Mchanganyiko

MSCL kujenga meli ya mizigo, abiria kwenda visiwa vya Comoro na Shelisheli

Spread the love

 

KAMPUNI ya Huduma za Meli (MSCL) imesema kuwa ipo katika mipango ya kukarabati Meli 13 na Kujenga Meli mpya tisa (9) ifikapo mwaka 2025, lengo ni kuweza kukamata masoko ya kusafirisha abiria na Mizigo katika nchi za DRC, Uganda, visiwa vya Comoro na Shelisheli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Mwanza jana, Mkurugenzi Mkuu wa MSCL Eric B. Hamissi amesema kuwa kuanzisha safari za kwenda Visiwa vya Shelisheli na Comoro ni moja kati ya mipango mikubwa ambayo Kampuni ya Huduma za Meli imepanga kuteteleza ili kuweza kusafirisha abiria na mizigo kwenda nchi hizo.

Aliongezea kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa reli ya SGR, mizigo kutoka Tanzania itaweza kusafirishwa kirahisi mpaka Sudan ya Kusini.

Mkurugenzi Hamissi alisema kuwa mpaka kufikia mwaka 2017, MSCL ilikuwa na meli tano; MV.Umoja, MV Liemba, MV Clarias, MT Sangara na MV Songea ambazo zilizokuwa zinatoa huduma, katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.

“Mpaka kufika mwaka huu wa 2023, MSCL inamiliki meli 17 ambazo kati ya hizo Meli 9 zipo katika Ziwa Victoria, Meli 3 na Boti 1 katika Ziwa Tanganyika na Meli 5 katika Ziwa Nyasa,” alisema.
Alitabanaisha kuwa kwa sasa MSCL inahudumia visiwa vya ukerewe, Gana na Godziba kwa kutumia Meli za MV Butiama na MV Clarias.

Kujiunga kwenye taasisi zinazowakutanisha wadau mbalimbali wa biashara, mfano TPSF. Lengo kuu ni kuendelea kupata wateja wa kutumia meli zetu kusafiri na kusafirisha mizigo ndani na nje ya Tanzania.

Akiongea kuhusu mafanikio yaliyopatikana toka kuanza rasmi kutoa huduma mwaka 1997, Mkurugenzi huyo alisema: “Katika awamu ya kwanza ya mpango wa kufufua huduma za usafiri katika maziwa makuu kupitia MSCL, Serikali ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili utekelezaji wa miradi mikubwa minne katika Ziwa Victoria.”

Aliongeza: “Miradi hiyo ni ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza “Hapa Kazi Tu”, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria ambayo imefikia asilimia 92, kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 107 na kutekelezwa na mzabuni GAS Entec.”

Aliendelea kuelezea kuwa ukarabati wa Meli za MV Victoria na Ukarabati wa meli ya MV Butiama ulikamilika mwezi Aprili, 2020 na Meli hizo zinaendelea kutoa huduma katika Ziwa Victoria.

“Miradi yote miwili ilikamilika kwa gharama ya Shilingi Bilioni 27.6 ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 22.7 ni kwa ajili ya ukarabati wa New Victoria Hapa Kazi Tu na Shilingi Bilioni 4.9 ni kwa ajili ya Ukarabati wa meli ya New Butiama Hapa Kazi Tu. Miradi hiyo imetekjelezwa na mzabuni KTMI Co. Ltd kutoka nchini Korea Kusini kwa kushirikiana na kampuni ya Yuko’s Enterprise (EA) ya Tanzania,” alisema Mkurugenzi Hamissi.

Aliendelea kuelezea kuwa ukarabati wa meli ya kubeba mabehewa (Wagon Ferry) ya MV Umoja unaotekelezwa na Kampuni ya SM SOLUTION CO. LTD ya Korea Kusini, ulikamilika mwezi Septemba, 2023. Meli hii imekarabatiwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani 8,422,840 ambazo ni sawa shilingi 19,811,446,192.40.

Alisisitiza kuwa MSCL katika kutekeleza miradi ya ukarabati wa meli chakavu, kwa sasa inatekeleza miradi ya ujenzi wa meli ya MV Mwanza katika ziwa Victoria, ukarabati umefikia asilimia 92.

“Miradi mingine inayotekelezwa hivi sasa ni pamoja na ukarabati wa meli ya mafuta ya MT Sangara katika ziwa Tanganyika, ukarabati umefikia asilimia 92, ukarabati wa meli ya MT Ukerewe katika ziwa Victoria, tayari mkataba umeishasainiwa kwa ajili ya utekelezaji pamoja na ukarabati wa meli ya mafuta ya MT Nyangumi katika ziwa Victoria, tayari mkataba umeishasainiwa kwa ajili ya utekelezaji,” alisema.

Miradi mingine aliyosema inaendela na utekelezwaji ni pamoja na ukarabati wa meli ya MV Liemba katika ziwa Tanganyika, tayari mkataba umeishasainiwa kwa ajili ya utekelezaji.

“Vile vile tupo katika tathmini ya kuweza kuweza kufanya ukarabati wa meli ya MV Mwongozo katika ziwa Tanganyika, ili kubaini aina ya matengenezo yanayohitajika katika meli hiyo,” alisema.
Alifafanua kuwa ukarabati wa mradi wa boti ya uokozi ya Sea Worriors  katika ziwa Tanganyika upo katika hatua za manunuzi.

Alieleze baadhi ya mikataba ambayo MSCL imeingiana kwa mwaka 2023 ni pamoja na mkataba wa Ujenzi wa Karakana ya kujengea meli (shipyard) katika Ziwa Tanganyika, Karakana hiyo itakuwa na eneo lenye urefu wa mita 188 na upana wa mita 140 na itakuwa na ukubwa wa mita 55,000 za mraba.

Alisisitiza: “Vilevile kwa mwaka 2023, tumeweza kuingia katika makubaliano ya mradi wa Ujenzi wa meli ya kubeba mizigo (Ro-Ro & Wagon Ferry) katika Ziwa Tanganyika Mzabuni wa kutekeleza mradi huu ni Kampuni ya DEARSAN SHIPYARD ya Uturuki kwa gharama za Dola za Marekani 63,467,143.00 (sawa na shilingi za kitanzania 158,274,361,213.40). Mradi huu utatekelezwa kwa muda wa miezi 36 kwa mujibu wa mkataba.”

Akizungumzia matarajio ya MSCL kwa mwaka 2024, Mkurugenzi Hamissi alisema: “Kwa mwaka 2024, zaidi ni utekelezaji na usimamizi wa Miradi tuliyoingia mikataba mwaka huu lakini pia kujiimarisha katika usafirishaji wa mizigo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati. Katika Mpango Mkakati, MSCL inatarajia kuwa na meli zisizopungua 22 ifikapo mwaka 2026.”

Akiongeza mafanikio ambayo MSCL inajivunia ni pamoja na  kurudisha Imani kwa serikali kutokana na utendaji bora na usimamizi mzuri wa miradi ya taasisi.

Akiongea kuhusu changamoto ambazo MSCL inapambana nazo ni pamoja na uchache wa meli zinazofanya kazi kwa sasa ambapo mpaka hivi sasa Kampuni ina meli saba (7) zinazofanya kazi hii ikijumuisha na meli ya mizigo – MV Umoja iliyoanza safari za majaribio mwezi Oktoba 2023. “Idadi hii ni ndogo sana kwa MSCL kujitegemea lakini vilevile kutoa mchango wake katika usafirishaji utakaoleta tija katika uchumi wa Taifa.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

RPC Dodoma akabidhiwa bunduki mbili za wahalifu

Spread the love  Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yazindua huduma maalum kwa wastaafu

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua huduma maalum kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yazindua akaunti ya Kikundi

Spread the loveBenki ya NMB imezindua akaunti ya kikundi yenye  maboresho makubwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyakazi waidai STAMICO mishahara ya bilioni 1

Spread the loveWALIOKUWA wafanyakazi wa mgodi wa Shirika la Madini la Taifa...

error: Content is protected !!