December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Matumaini mapya mgawo wa maji Dar

Spread the love

 

MACHUNGU ya mgawo wa maji kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania yaliyodumu kwa takribani wiki tatu, yanaanza kupungua kuanzia leo Jumatatu, tarehe 22 Novemba 2021, baada ya kina cha maji katika mto wa Ruvu kuongezeka. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ni baada ya mafanikio ya operesheni iliyoelekezwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa wasimamizi wa Bonde la Mto Ruvu kufuatilia njia zote za kuingiza maji katika mto huo zilizochepushwa ziwe wazi.

Majaliwa alitembelea Mto Ruvu tarehe 15 Novemba 2021 na kutoa siku tatu kuanzia siku hiyo baada ya mgawo huo wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam kuilalamikia Serikali kushindwa kutatua changamoto hiyo.

“Tumieni sheria iliyoanzisha mamlaka yenu kuhakikisha mnailinda mito na maziwa,” alisema Majaliwa

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa jijini Mwanza, tarehe 18 Novemba 2021 kwenye maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Hospitali ya Bugando, alitoa maagizo kwa mamlaka zote nchini kufuatilia wahujumu wa vyanzo vya maji ili waweze kuchukuliwa hatua madhubuti.

Juzi usiku Jumamosi tarehe 20 Novemba 2021, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwa na viongozi mbalimbali wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) akiwemo afisa mtendaji wake mkuu, Mhandisi Cyprian Luhemeja walitembelea mtambo wa Ruvu.

Mhandisi Cyprian Luhemeja

Mhandisi Luhemeja alipongeza maagizo ya Rais Samia na Waziri Mkuu, Majaliwa kwani yamezaa matunda na kusaidia kuongeza kina cha maji kwani “wakulima na wafugaji walikuwa wamevamia vyanzo vya maji.”

“Naweza kusema kwa sasa huduma ya maji imerejea vizuri, mto umejaa maji, tunaweza kuzalisha,” alisema Mhandi Luhemeja

Alisema, waziri mkuu Majaliwa alipowatembelea Jumatatu iliyopita, “kina cha maji kilikuwa chini sana ya mita 0.1 na sasa kipo mita 1.6 ambayo n iminium tunayoweza kuzalisha.”

Mhandisi Luhemeja alisema, “uwezo wa mtambo kwa sasa kwa saa 24 unatoa lita milioni 230, wakati waziri mkuu anatutembelea ulikuwa chini sana. Matanki yamekwisha kujaa, kipande cha Bagamoyo hadi katikati ya Jiji kinapata maji.”

Kuhusu watumiaji wabaya wa maji kama wafugaji, wakulima kwa kushirikiana na viongozi wengine “umesaidia sana kuongeza kina cha maji. Leo (juzi) tuko normal na kufikia kesho (jana) jioni hali itakuwa kawaida na maji yataanza kupatikana.”

Awali, Waziri Aweso alisema “tunatambua mvua zimechelewa kunyesha lakini shughuli za kibinadamu nazo zimeathiri sana na kama wananchi tunapaswa kujifunza.”

Juma Aweso, Waziri wa Maji

“Suala la kulinda na kutun za vyanzo vya maji, suala la kulinda na kutunza mazingira ni la kila mmoja si sisi viongozi. Kila mmoja wetu anapaswa kulinda mazingira na vyanzo vya maji,” alisema

Waziri huyo aliwaonyooshea kidole, viongozi wa bonde akisema “lazima wajitathimini na tupimane uwezo wetu. Si kukaa ofisini ni kila mmoja kutumiza wajibu wao.”

Aliwapongeza watendaji mbalimbali kwa kujitoa kwao “na mimi niwaombe wananchi, kunapotokea matatizo tuwe pamoja na kuwatia moyo. Tushikamane. Watu wanakesha hapa mtamboni kuhakikisha tunapata maji.”

“Hiki ni kipindi cha mpito, twendeni tukahifadhi maji, tutumie vizuri nah ii rasilimali ndogo tuliyoipata wana Dar es Salaam, Pwani na maeneo mengine tuhakikishe tunalinda vyanzo,” alisema

Waziri Aweso aliiagiza DAWASA kuhakikisha inatoa ratiba sahihi ya mgao wa maji “kama ukisema Magomenbi watapata maji siku hii na yatoke” huku viongozi wa bonde wasimamie sheria na si kuonekana haya.

“Lakini nawashukuru sana Bodi ya DAWASA, ndugu yangu Luhemeja hongesa sana, unashinda hapa na timu yako. Mnafanya kazi nzuri na sisi tupo pamoja.”

“Baada ya kumaliza hii changamoto, nitaomba kukutana na timu nzima waliombana usiku na mchana ili kutoa shukurani za dhati kuhakikisha wananchi wanapata maji,” alisema

error: Content is protected !!