December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Mbowe kuendelea leo, uamuzi wa pingamizi wasubiriwa

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu tarehe 22 Novemba 2021, itatoa uamuzi mdogo katika kesi ya ugaidi dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Uamuzi huo wa pingamizi la utetezi, waliloweka dhidi ya kielelezo kilichowasilishwa na shahidi wa Jamhuri katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, itatolewa na Jaji Joachim Tiganga anayeisikiliza.

Pingamizi hilo dhidi ya kitabu cha kumbukumbu ya mahabusu (DR) kutoka Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, likitaka kisipokelewe mahakamani hapo kama ushahidi, lilikuja baada ya kuwasilishwa na shahidi Koplo Mpelelezi Ricardo Msemwa.

Msemwa ambaye kituo chake ni Oysterbay, aliwasilisha kitabu hicho Jumatano iliyopita katika Mahakama hiyo wakati akitoa ushahidi wake.

Mawakili wa utetezi, waliweka pingamizi hilo wakati shahidi huyo akitoa ushahidi katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshitakiwa, Mohamed Ling’wenya yasipokewe wakidai hakuyatoa akiwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam wala Kituo cha Polisi Mbweni jijini humo.

Jopo la mawakili wa utetezi linaloongozwa na Peter Kibatala akisaidiana na Jeremiah Mtobesya, lilitoa hoja tatu katika pingamizi hilo, likidai kitabu hicho kilikwishatolewa uamuzi katika kesi kama hiyo ya Adam Kasekwa, lakini utaratibu haukufuatwa kukipata, na Mahakama haijatoa amri ya kitabu hicho kutoka.

Mbali na Mbowe, Ling’wenya na Kasekwa, mwingine ni Halfan Bwire ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kwa tuhuma za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi nchini.

Pingamizi hilo, lilishuhudia mawakili wa pande zote mbili wakitumia siku mbili za Jumatano na Alhamisi iliyopita wakichuana vikali na Jaji Tiganga kutumia siku ya Ijumaa kuandika uamuzi ambao alisema, atautoa leo.

Kesi hiyo ya aina yake kuwahi kutokea nchini kwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi.

Katika mapingamizi yaliyowekwa tangu kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo mwishoni mwa Agosti mwaka huu, mapingamizi saba yametupwa, huku upande wa kina Mbowe ukiambulia kushinda mawili pekee.

Miongoni mwa mapingamizi yaliyotupwa; ni uhalali wa Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo, maelezo ya onyo ya mshitakiwa Kasekwa yasipokewe, na hati iliyotumika kufungua kesi hiyo kuwa na makosa ya kisheria.

Jingine, ni hati ya ukamataji mali za washitakiwa Kasekwa na Ling’wenya iliyowasilishwa mahakamani isipokewe na lile lililohusu usahihi wa saini ya shahidi wa nne wa Jamhuri, Anita Mtaro (45), mfanyabiashara wa mbege, Rau Madukani, Moshi, Kilimanjaro.

Upande wa utetezi, ulitaka shahidi huyo asaini pembeni, ili kulinganisha saini alizokuwa amesaini katika fomu zilizotumika kujaza vitu walivyokutwanavyo Kasekwa na Lingw’enya baada ya kukamatwa Rau Madukani.

Pingamizi jingine lililotupwa, lilihusu shahidi wa Jamhuri, Msemwa kukutwa kizimbani akiwa na simu, kalamu na shajara.

Mapingamizi ambayo Mbowe na wenzake walishinda, ni kitabu cha kumbukumbu cha mahabusu, chenye taarifa za mshitakiwa Ling’wenya aliyewekwa mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.

Kitabu hicho kiliombwa na shahidi wa Jamhuri, askari Polisi Jumanne Malangahe kipokewe, lakini hakikupokewa kwa sababu hakuonesha jinsi kilivyomfikia.

Pingamizi la pili, lilihusu nyaraka iliyowasilishwa mahakamani hapo ikionesha jinsi Mbowe aliyewahi kuwa Mbunge wa Hai, alivyokataa kutoa maelezo yake huku akikubali kusaini. Nyaraka hiyo haikupokewa.

error: Content is protected !!