Saturday , 27 April 2024
Home Kitengo Michezo Mashindano ‘NBC Waitara Trophy 2024’ yang’ara
Michezo

Mashindano ‘NBC Waitara Trophy 2024’ yang’ara

Spread the love

Mashindano ya Gofu ya ‘NBC Waitara Trophy 2024’ yamehitimishwa kwa mafanikio makubwa huku mdhamini mkuu wa mashindano hayo, benki ya NBC ikiahidi kuendelea kuyaboresha zaidi mashindano hayo ili yaendelea kuwa chachu ya kukuza na kuendeleza vipaji vya mchezo wa golf.

Pia imeahidi kutumia mashindano hayo kutangaza utalii sambamba na kumuenzi muasisi wa mashindano hayo Mkuu wa majeshi Mstaafu, Jenerali George Waitara. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ni alikuwa mmoja wa wakishiriki wa mashindano ya Gofu ya NBC Waitara Trophy.

Mashindano hayo yaliyohitimishwa na muasisi wake Jenerali Waitara kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu vya Lugalo Jijini Dar es Salaam jana Jumatatu yalihusisha washiriki takribani 122 kutoka ndani na nje ya nchi, ikishuhudiwa wachezaji wa klabu ya gofu  Lugalo waking’ara zaidi huku mchezaji Boniface Japhet kutoka klabu hiyo akiibuka mshindi wa jumla wa mashindano hayo.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi mbalimbali wa mashindano hayo, Jenerali Waitara pamoja na kuwapongeza washiriki na wadhamini wa mashindano hayo, alitoa wito kwa jamii kushiriki kwa wingi kwenye mchezo huo unaojiongezea umaarufu hapa nchini.

Pia aliwasihi wapuuzie dhana iliyojengeka kwa muda mrefu kuwa mchezo wa gofu ni mahususi tu kwa watu wenye kipato kikubwa kwenye jamii.

“Niwasihi sana wazazi muendelee kuwaruhusu watoto na vijana wenu wajitokeze kwa wingi kushiriki mchezo huu kwa kuwa mbali na sababu za kiafya pia umekuwa ukiambatana na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa washiriki huku pia ukitoa wasaa kwa washiriki kukutana na watu wa aina mbalimbali ndani na nje ya nchi hatua ambayo imekuwa ikiwasaidia kufungua fursa mbalimbali za kijamii na kibiashara,’’ alisema.

Zaidi Jenerali Waitara alitoa wito kwa wadhamini wa mashindano mbalimbali ya mchezo huo yakiwemo mashindano hayo kuangalia namna ya kupanua udhamini wao mbali na mashindano pekee pia waone namna ya kuboresha viwanja vya mchezo huo hususani kwenye mfumo wa umwagiliaji ili viweze kuwa katika hali nzuri hata kwenye msimu wa ukame.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Wateja wadogo na Binafsi  wa benki ya NBC, Elibariki Masuke, Mkuu wa Idara ya Bima, Benki ya NBC, Benjamin Nkaka alisema  ushiriki wa benki hiyo kwenye mashindano hayo kwa kiasi kikubwa unasukumwa na adhma ya benki hiyo katika kukuza na kuendeleza sekta ya michezo nchini ili kuibua vipaji, kuchochea ajira kupitia michezo pamoja na kuitumia vema sekta hiyo katika kutangaza utalii wa ndani.

Jenerali Waitara akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi mbalimbali wa mashindano hayo.

“Kwetu mchezo wa gofu tunautazama kama moja ya michezo ya kimkakati inayoweza kulitangaza zaidi taifa hili huku pia ukitoa fursa kwa makundi tofauti ya wana jamii kuweza kujijengea fursa tofauti zikiwemo zile za kiuchumi bila kujali umri, jinsia au daraja lolote kiuchumi.

“Tumeamua kuunga mkono jitihada za muasisi wa mashindano haya Jenerali Waitara tukitambua hilo. Tunaahidi kuendeleza uhusiano wetu huu mzuri kupitia mashindano haya ili yaweze kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake,’’ alisema Nkaka.

Akizungumzia mashindano hayo, Meneja wa Klabu ya Jeshi la Ulinzi la wananchi Wa Tanzania ya Lugalo-JWTZ Kanali David Mziray alisema licha ya kufanyika kwa mafanikio imeshuhudiwa washiriki mbalimbali wakiwemo watoto wakifanya vizuri zaidi kwenye mashindano hayo kwa kupata alama nzuri zaidi hatua ambayo inawakikishia ujio wa vipaji bora zaidi katika wakati mfupi ujao.

Mkuu wa Idara ya Bima, Benki ya NBC Benjamin Nkaka akizungumza kwenye hafla hiyo.

“Kupitia mashindano haya tumeshuhudia watoto wakifanya vema zaidi kwenye baadhi ya maeneo kiasi ambacho alama zao zinatoa changamoto kwa wakubwa hususani kwenye eneo kama upigaji wa mipira mirefu, hatua ambayo inatuonyesha mwanga mzuri huko tuendapo.

“Katika kuhakikisha hili linafanikiwa klabu yetu ya Lugalo tunatoa mafunzo ya mchezo wa gofu kwa watoto bure katika siku zote za Jumamosi,’’ alibainisha.

Mwalimu wa mchezo wa golf kutoka klabu ya Lugalo, Abdallah Sanzagala (Pro Dullah) akiwaelekeza baadhi ya wafanyakazi wa benki ya NBC namna bora ya kucheza mchezo huo. Anayeshuhudia ni Mkuu wa Idara ya Bima, Benki ya NBC Bw Benjamin Nkaka (Kulia) ambaye ni moja ya wachezaji vinara wa mchezo huo.

Kwa upande wao Rais wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Gilman Kasiga na Rais wa chama cha gofu cha wanawake Tanzania (TLGU), Queen Siraki pamoja na kuonyesha kuvutiwa kwao na mafanikio makubwa ya mashindano hayo yanayoboreshwa kila mwaka walivutiwa zaidi na ongezeko kubwa la ushiriki wa wanawake na Watoto kwenye mashindano hayo hatua ambayo walisema inathibitisha muamko wa wana jamii katika kuupokea mchezo huo.

“Hata hivyo ushiriki wa ‘seniors’ sio mzuri sana hivyo tunaomba vilabu vione ipo haja ya kuanzisha mashindano maalumu kwa ajili ya seniors ili kuchochea ushiriki wao sambamba na kutoa fursa  ya wao kukutana na kukumbushana mambo mbalimbali…hiyo ni miongoni mwa malengo ya mchezo huu,’’ alisema Kasiga.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Michezo

EPL, Ligue 1 na Coppa Italia kinawaka leo

Spread the love  LEO ligi kadhaa zitaendelea nchini barani ulaya ikiwemo ligi...

BiasharaMichezo

NBC yaunga mkono jitihada kutokomeza malaria

Spread the loveKuelekea Maadhimisho ya siku ya malaria Duniani yatakayofanyika kesho Aprili...

Michezo

Arsenal dhidi ya Chelsea ngoma nzito leo EPL

Spread the love  Leo kutakua na mchezo mkali sana pale kwenye ligi...

Habari MchanganyikoMichezo

NBC yanogesha Derby Kariakoo, Aziz Ki aibuka mchezaji bora Machi

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambayo ni mdhamini Mkuu...

error: Content is protected !!