MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ametoa siku kumi kwa uongozi wa Manispaa ya Kigamboni kuhakikisha Hospital wilaya hiyo inaanza kutoa huduma kwa wananchi ifikapo tarehe 1 June, 2020 baada ya Majengo yote ya Hospital hiyo kukamilika. Anandika Hamis Mguta, Dar es salaam…(endelea).
RC Makonda ametoa agizo hilo leo Ijumaa tarehe 22 Mei, 2020 wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo.
Katika ziara hiyo, Makonda amekabidhi Magodoro 175, Mashuka 1,294 na Ndoo na kueleza ifikapo Jumanne ya wiki ijayo atakabidhi tena Mashine mbili za Ultrasound zenye thamani ya Sh. 70 milioni na Vitanda 100 ili kuhakikisha huduma zinaanza kutolewa.
Aidha RC Makonda amemuelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa huo kuhakikisha anapeleka watumishi 40 kwenye hospital hiyo kwaajili ya kutoa huduma ili kutimiza lengo la Serikali ya Awamu ya Tano la kupunguza kero za Afya kwa Wananchi.
Hospitali mpya ya wilaya ya Kigamboni
Akiwa katika ukaguzi wa Ujenzi wa Barabara na Round about inayounganisha barabara za kuelekea Feri na Kibada kutokea Daraja la Mwalimu Nyerere, Makonda amewaelekeza Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) kuhakikisha ujenzi wa barabara na mzunguko wa magari vinakamilika na kukabidhiwa kabla ya Septemba 2020.
Pamoja na hayo, Makonda amewaelekeza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Watendaji wa Jiji hilo kuhakikisha maelekezo na ahadi zote zinazotolewa na Rais John Magufuli vinatekelezwa kwa wakati pasipo kushurutishwa huku akiwataka Wakandarasi wote kuhakikisha miradi yao inakamilika kwa wakati.
Leave a comment