KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) nchini Tanzania, imeishauri Serikali kuhakikisha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), linalipwa fedha zaidi ya Sh. 454 bilioni, inazodai kutoka taasisi za umma na wateja binafsi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Hayo yamesemwa leo Ijumaa tarehe 22 Mei 2020, bungeni jijini Dodoma na, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly wakati anawasilisha taarifa ya kamati hiyo, kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2019.
Hilaly amesema, kwa mujibu wa taarifa ya CAG, hadi kufikia tarehe 30 Juni 2019, TANESCO inadai taasisi za Serikali Sh. 205.8 bilioni, wateja binafsi Sh. 199.3 na madeni mengine Sh. 49 bilioni.
Amesema, deni hilo linasababisha hali ya ukwasi ya shirika hilo kupungua na kuathiri utendaji wake, ikiwemo kugharamia shughuli mbalimbali.
Hilaly ambaye ni mbunge wa Sumbawanga Mjini kupitia CCM amesema, PAC imeishauri Serikali ichukue jitihada mahsusi za kibajeti kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, kuhakikisha taasisi zote za serikali zinazodaiwa na TANESCO zinalipa madeni yao.
“Serikali ichukue jitihada mahsusi za kibajeti kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na TANESCO zinalipa madeni yao kwa kuzingatia utaratibu wa kibajeti utakaowekwa na Hazina,”amesema Hilaly
Aidha, Hilaly amesema, Bunge limeshauri uongozi wa TANESCO, uimarishe mikakati ya ukusanyaji madeni ili fedha hizo zipatikane kwa wakati.
“Uwepo wa deni hilo, unaathiri hali ya utendaji wa kila siku wa TANESCO na unaharibu taswira halisi ya taarifa za hesabu za shirika, kwa hiyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Menejimenti ya TANESCO iimarishe mikakati ya ukusanyaji wa madeni ili kuhakikisha madeni husika yanakusanywa kwa wakati,” amesema.
Leave a comment