November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa: Vijiji 10,361 vyafikishiwa umeme, bado 1,956

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme hususan maeneo ya vijijini ambapo hadi sasa jumla ya vijiji 10,361 kati ya vijiji 12,317 vya Tanzania Bara sawa na asilimia 84.12 vimeunganishiwa umeme. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha hadi kufikia Desemba 2022 vijiji 1,956 vilivyosalia vinapata umeme kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ulioanza kutekelezwa Julai, mwaka huu. Gharama za mradi huu ni shilingi trilioni 1.24,” amesema

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, tarehe 12 Novemba 2021, wakati akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa tano wa Bunge la 12 la Tanzania jijini Dodoma hadi Jumanne ya 1 Februari 2022.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji na usambazaji umeme maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha maeneo yote ya mijini na vijijini yanapata umeme wa kutosha, nafuu na uhakika.

Majaliwa ametaja baadhi ya miradi ya kimkakati ya uzalishaji umeme kuwa ni mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (MW 2,115) ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 55.6 na mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Rusumo (MW 80) uliofikia asilimia 81.2.

Vilevile, Majaliwa amesema Serikali imekamilisha mradi wa njia ya kusafirisha umeme (KV 220) kutoka Bulyanhulu hadi Geita wenye urefu wa kilomita 55. Miradi mingine ya kusafirisha umeme inayoendelea kutekelezwa ni kutoka Rusumo kwenda Nyakanazi kupitia Benaco (KV220), Tabora kupitia Urambo – Nguruka hadi Kidahwe (KV 132) na Tabora hadi Katavi kupitia Ipole na Inyonga (KV132).

“…Serikali inaendelea na maandalizi ya mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 400 kutoka Iringa – Mbeya – Tunduma hadi Sumbawanga na mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa KV 400 kutoka Sumbawanga – Mpanda hadi Kigoma.”

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo ya uzalishaji na usambazaji umeme kutawezesha maeneo yote nchini kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa na hivyo kupata huduma ya uhakika ya umeme.

error: Content is protected !!