September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Machinga Dar wamwomba JPM awasaidie

Makamu Mwenyekiti wa Machinga Taifa, Steven Lusinde (aliyesimama)

Spread the love

WAJASIRIAMALI wadogo maarufu ‘machinga’ eneo la Gongolamboto wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, wamemmwomba, Rais John Magufuli wa Tanzania kutatua mgogoro wa ulinzi shirikishi uliodumu kwa miezi mitano kati ya serikali ya mtaa huo na uongozi wa machinga. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wamesema, mgogoro huo umesababisha baadhi ya wafanyabiashara kupigwa na kuporwa bidhaa zao.

Kilio hicho, walikitoa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati aa mkutato wa dharura ulioitishwa na uongozi wa Taasisi ya Umoja wa Wajasiliamali wadogo wadogo Gongolamboto (GOWASO).

Walisema mgogoro huo umesababishwa watu kupigwa kutokana kila upande kati ya mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo na uongozi huo wakitaka kuweka ulinzi shirikishi.

Mmoja wa Wajasiliamali hao, Jonathan Kalingo alisema, kutokana na mgogoro huo, wafanyabiashara wamekuwa wakipigwa na kikundi cha ulinzi shirikishi kilichoundwa chini ya serikali ya mtaa huo.

“Tunamwomba Rais Magufuli aje Gongolamboto kutuondolea mgogoro kwa kuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa huu ameunda kikundi cha ulinzi shirikishi ambacho mara kwa mara wamekuwa wakiwapiga walinzi shirikishi wetu ambao tumewachagua chini ya uongozi wa polisi pamoja na uongozi wa machinga,” alisema Kalingo.

Baadhi ya wamachinga wakiwa katika mkutano

Alisema, kinachojitokeza mwenyekiti wa serikali ya mtaa amekuwa akiwadai wafanyabiashara kila mmoja atoe Sh. 300 kwa ajili ya ulinzi shirikishi lakini ulinzi ulioundwa na wamachinga hao walikubaliana kila mfanyabiashara atoe Sh.200 kwa ajili ya ulinzi.

Easter Hossea alisema, wanapokuwa kwenye biashara zao, wamekuwa wakisumbuliwa na walinzi shirikishi wa serikali ya mtaa huo pindi wanapowakatalia kuwa wao hawawatambui bali wanawatambua walinzi waliowachagua wao ndipo wanajikuta baadhi yao wakifanyiwa fujo huku bidhaa zao zikipotea.

Alipotafutwa Kwa njia ya simu mwenyekiti wa mtaa huo simu yake ilikuwa haipatikani lakini Mwenyekiti wa wenyeviti wa Kata ya Gongolamboto, Mohamed Mzala alikiri kuwepo kwa mgogoro huo.

Alisema, mwezi na nusu uliopita walifanya kikao ili kutatua mgogoro huo ambapo ilikuwepo kamati ya maendeleo ya Kata, mwenyekiti wa mtaa wa Gongolamboto pamoja na kamati yake, uongozi wa machinga,mkuu wa polisi wilaya ya Ukonga, mkuu wa Takukuru wilaya ya IIala, mkuu wa kituo cha polisi Gongolamboto na katibu tawala wa wilaya hiyo.

Mzala alisema, katika kikao kile walikubaliana wamachinga wakitaka kufanya lolote lazima waripoti kwa mwenyekiti wa mtaa huo ikiwemo makusanyo ya ulinzi yapitie kwenye serikali ya mtaa huo.

Alisema, katibu tawala wa wilaya hiyo aliwaagiza wamachinga hao kuwa walinzi wao wanaolinda waende serikali za mtaa ili washirikiane na walinzi wa serikali ya mtaa huo.

“Pia, katibu tawala alitoa maagizo kwa mkuu wa polisi wilaya ya kipolisi Ukonga, Takukuru wakae na hao machinga kwa ajili ya kuwahoji na baadaye warudishe mrejesho kwake,”amesema

Makamu mwenyekiti Taifa wa Machinga nchini, Steven Lusinde aliwataka walinzi waliokuwa wakilinda maeneo hayo waendelee kuulinda kwa kujitolea wasichukue fedha yeyote kwa wafanyabiashara hao hadi hapo mgogoro huo watakapoumaliza.

Naye mwenyekiti wa Machinga Gongolamboto, Christofa Kidiga alisema, kikao hicho kilikuwa cha kikatiba kwa ajili ya kuzungumzia maendeleo yao.

error: Content is protected !!