Saturday , 3 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu amwambia Waitara, walionishambulia niliwaona
Habari za SiasaTangulizi

Lissu amwambia Waitara, walionishambulia niliwaona

Spread the love

BAADA ya aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Mwikabe Waitara kuzungumzia tukio la kushambuliwa kwa Tundu Lissu, tarehe 7 Septemba mwaka jana, Mbunge huyo wa Singida Mashariki, ametoa ya moyoni kuhusiana na tukio hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Lissu ambaye hakuwa kuelewa kilichotokea katika tukio lake, lakini amelamizika kueleza baada ya kusikia upotoshaji wa Waitara.

Mbunge huyo ameandika akiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu amesema waliomshambulia aliwaona kwa macho yake na anajua kila kilichotokea siku hiyo.

Hana chini ni ujumbe aliouandika Lissu:

Nimemsikia Mwita Mwikabe Waitara na alichokisema juu ya jaribio la mauaji dhidi yangu la September 7 mwaka jana.

Sijashangazwa hata kidogo na maneno yake. Amerudi kwenye madhehebu yake ya zamani, lazima ajionyeshe ana msimamo mkali wa kiimani kuliko wale aliowakimbia mwanzoni na ambao sasa amewarudia.

Nilishambuliwa nikiwa na dereva wangu. Niliwaona walionishambulia kwa macho yangu mwenyewe.

Niliona alichofanya dereva wangu kuanzia risasi zinarushwa mpaka aliporuka nje ya gari na kujificha.

Niliona jinsi yeye na mfanyakazi wangu wa nyumbani wakisaidiana na mfanyakazi wa Naibu Spika Tulia walivyonitoa kwenye gari yangu na kunikimbiza hospitalini kwenye gari ya mfanyakazi wa Naibu Spika Tulia.

Mimi ndiye niliyemwagiza ampigie simu Mwenyekiti Mbowe na wabunge wengine wa CHADEMA wakati wananikimbiza hospitali. Nilikuwa na fahamu na nilikuwa nazungumza mpaka nilipoingizwa theatre Dodoma General Hospital.

Nimekaa na dereva wangu miezi minne Nairobi Hospital. Polisi walileta ujumbe kwamba wanataka kuja kunihoji mimi na dereva wangu.

Tuliwaambia waje. Hawakuonekana mpaka tumeondoka Kenya na kuja Ubelgiji. Leo hii ni miezi saba tangu tuje Ubelgiji. Hawajaonekana.

Tuna uhusiano wa kibalozi na Ubelgiji wa miaka mingi. Wana Ubalozi kwetu na tuna Ubalozi hapa kwao. Serikali ya Magufuli haijaomba msaada wa Serikali ya Ubelgiji ili utaratibu wa kumhoji huyu dereva au mimi mwenyewe ufanyike.

Tuna sheria iliyotungwa na Bunge letu inayoitwa Mutual Assistance in Criminal Matters Act, ambayo imeweka utaratibu wa nini kifanyike mtuhumiwa wa jinai au shahidi anapokuwa kwenye nchi nyingine. Hakuna mwenye habari nayo.

Jeshi la Polisi la Tanzania ni mwanachama wa Interpol (International Police Organization) ambayo inaweza kusaidia upelelezi wa jambo hili. Interpol nayo imesahaulika.

Dereva wangu amesafiri mchana kweupe kutoka Dodoma hadi Nairobi. Ametumia hati ya muda ya kusafiria iliyotolewa na watumishi wa Idara ya Uhamiaji ya Tanzania mpakani Namanga.

Amekuja Ubelgiji kwa hati ya muda ya kusafiria iliyotolewa na Ubalozi wa Ubelgiji Nairobi kwa sababu hati ya muda ya Tanzania ilikwisha muda wake.

Anaishi Ubelgiji mchana kweupe. Niko naye muda mwingi. Aliyekuwa Balozi wetu hapa na maafisa Ubalozi wa kwetu wamenikuta naye hospitali. Nimemtambulisha kwao.

IGP Sirro alishasema hadharani kwamba Jeshi la Polisi limefunga faili la upelelezi juu ya kushambuliwa kwangu. Polisi wanajua kilichofanyika, ndio maana hawajawahi kuhangaika na taratibu hizi za kufahamu ukweli.

CHADEMA na familia yangu tulidai uchunguzi huru wa shambulio dhidi yangu. Tulisema Serikali ya Magufuli na watu wake wanahusika na jaribio la mauaji dhidi yangu. Hawawezi na hawataweza kujichunguza.

‘Watu wasiojulikana’ walitumwa kuja kuniua. Ndio maana ulinzi wote Area D ninapokaa uliondolewa siku hiyo.

Ndio maana CCTV ya kwa Waziri wa Nishati Medard Kalemani iliondolewa baada ya tukio.

Ndio maana Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama ilizuiliwa kuwasilisha taarifa yake bungeni.

Ndio maana Magufuli aliwakataza Wabunge wa CCM na viongozi wa serikali kuja kuniona hospitalini Nairobi.

Ndio maana amekataza Bunge la Spika Ndugai kunitibu kama inavyotakiwa na Sheria ya Uendeshaji wa Bunge.

Ndio maana sasa tunasikia kwamba mara baada ya kushambuliwa, Magufuli aliwaelekeza Mawaziri Mwigulu Nchemba na Augustine Mahiga kukanusha hadharani kwamba Serikali yake haikuhusika na jaribio hilo la mauaji.

Ndio maana tunasikia kulitolewa maagizo, mara baada ya kushambuliwa kwangu, kwamba nikifariki dunia mwili wangu ukimbizwe haraka kwetu Ikungi, Singida, kwa maziko; kusiwe na shughuli yoyote rasmi bungeni Dodoma, na kwa vyovyote vile nisipelekwe Dar yaliko makazi yangu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Bosi NIC apandishwa kizimbani, akabiliwa na mashitaka 365

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa...

Habari za Siasa

Lusinde: CCM hatuliachii ng’o jimbo la Moshi Mjini

Spread the loveMJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Livingston...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar: Bakharesa hajavamia shamba letu

Spread the love  IKULU Visiwani Zanzibar, imeeleza kuwa eneo la kiwanda cha...

Habari za SiasaTangulizi

Zanzibar watangaza rasmi kuwa shamba la Razaba ni mali yao

Spread the love  SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetangaza rasmi kwamba shamba...

error: Content is protected !!