Saturday , 27 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Jukwaa la wahariri lasikitishwa waandishi kushambuliwa, laonya wasiasa kuhamasisha vurugu
Habari MchanganyikoTangulizi

Jukwaa la wahariri lasikitishwa waandishi kushambuliwa, laonya wasiasa kuhamasisha vurugu

Spread the love

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limesikitishwa na tukio lililofanywa na vijana wa Kimasai (morani) zaidi ya 200 katika Kata ya Enduleni, wilayani Ngorongoro la kuwashambulia waandishi wa habari na kuwatia majeraha makubwa wakiwa kazini. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

TEF imetoa tamko hilo baada ya jana tarehe 15 Agosti 2023, vijana hao wakiwa na silaha za jadi (mapanga, mikuki, sime na mishale), kuwavamia wanahabari wakati wanakusanya taarifa kutoka kwa Wamasai wanaoishi Ngorongoro wanaotaka kuhama kwa hiyari kutoka katika Kijiji cha Enduleni kilichopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Arusha kuelekea kuishi Msomera wilayani Handeni, Tanga.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile imewataja waandishi wa habari waliofikwa kuwa ni mkasa huo ni Ferdinand Shayo (ITV), Denis Msacky (Media Brain), Habib Mchange (Jamvi la Habari), Elia Kinian (Channel Ten), Janeth Joseph (Mwananchi), Dickson Busagaga (Clouds Media) na mkalimani wao Lengai Ngoishiye.

Baada ya wanahabari hao kushambuliwa, walipelekwa kupata matibabu katika Hospitali ya FAME iliyopo Karatu.

Imesema waandishi hao wanamtuhumu Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangai kuwa alimtuma Katibu wake wakati yuko mnadani na Diwani kuwatawanya wananchi wasizungumze na waandishi wa habari. Baada ya kuona wananchi hao hawatii katazo lake, akawaashiria vijana wa Kimasai washambulie waandishi hao wa habari.

“Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) linakemea vikali tukio hili la kijinai lililolenga kuwaumizi waandishi wa habari waogope kufanya kazi yao ya kuhabarisha wananchi.

“TEF pia inakemea hatua ya wanasiasa kuhamasisha wananchi kujichukulia sheria mkononi. Imekuwa kawaida baadhi ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kuwaambia Wamasai kuwa adui yao mkubwa ni vyombo vya habari nchini na sasa kauli hizi zimethibitishwa kwa tukio hili la kijinai.

“Kazi ya uandishi wa habari hatuifanyi kwa hisani bali ni haki ya Kikatiba inayotolewa chini ya Ibara ya 18 ya Katiba yaTanzania (1977) na Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016) kama ilivyorekebishwa mwaka 2023. Kwa namna yoyote, ile ni kinyume cha Katiba na Sheria za nchi kuwashambulia waandishi wakiwa wanatekeleza majukumu yao,” imesema.

TEF imeomba Jeshi la Polisi kuchunguza, kuwasaka na kuwakamata wote waliohusika na shambulio hilo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

Aidha, imewaonya wanasiasa wanaotumia shida za wananchi, uelewa mdogo wa wananchi na hila kujitengenezea umaarufu kwa kuwahadaa wananchi kuwa wanawatetea wabaki Ngorongoro, ilihali moyoni wakifahamu fika kuwa wanahatarisha maisha ya wapigakura wao waendelee kuliwa na wanyama.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, TEF inafuatilia kwa karibu mfululizo wa matukio ya kushambuliwa waandishi wa habari, kuwadhalilisha kwa kuwatenga katika makundi ya “waandishi wa kisasa” na “wa zamani”, manyanyaso na matusi kwa waandishi kupitia mitandaoni, ambapo tunawasihi wananchi na viongozi wenye hulka hizo kuziacha mara moja kwani hazina afya kwa maendeleo ya taifa letu.

“TEF tunasubiri kusikia hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya watu hawa wanaofanya vitendo vya kihuni visivyokubalika katika utawala wa sheria. Ni matarajio yetu, watuhumiwa wote watakamatwa na watachukuliwa hatua za kisheria ili iwe funzo kwa wengine,” imesema taarifa hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

error: Content is protected !!