WANACHAMA wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wamemchagua Afisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Morgage Refinance Company Limited – TMRC, Oscar Mgaya kuwa mwenyekiti mpya wa Bodi ya chama hicho- ATE kwa kipindi cha miaka mitatu (2023-2026). Anaripoti Gabriel Mushi…(endelea).
Mgaya amechukua nafasi ya Mwenyekiti Jayne Nyimbo ambaye amemaliza muda wake.
Mgaya amechaguliwa leo tarehe 22 Juni 2023 katika mkutano mkuu wa 64 wa chama hicho uliuofanyika jijini Dar es Saalam.
Katika mkutano huo pia wanachama wamemchagua Imelda Lutebinga ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa G4S Secure Solutions Tanzania Ltd. kuwa Makamu Mwenyekiti wa ATE sambamba na wajumbe wa bodi ya chama hicho kutoka katika sekta 10.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti mpya wa ATE, Oscar Mgaya mbali na kuwashukuru wanachama wa ATE kuwa kumuamini, pia aliahidi kuendeleza ushirikiano na serikali pamoja na wadau wengine ikiwamo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA).
“Tunashukuru serikali kwa ushirikiano tunaoupata kwa mfano kupunguza skills levy kutoka asilimia 4 hadi 3.5… hakika tunashukuru serikali kwa kusikiliza na kufanyia kazi masuala ambayo ni muhimu kwa waajiri,” amesema.
Akizungumzia uchaguzi huo, Naibu Waziri ,Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi amewapongeza wanachama wa ATE kwa kufanikisha mabadiliko hayo bila kuwa na mushkeli.
Pia ATE imezindua progamu maalumu ya chama hicho (membership portal) ambayo itakuwa inapatikana kwenye simu rununu pamoja na kompyuta katika kuwawezesha wanachama kujisajili na kupata taarifa na huduma muhimu kwa njia ya mtandao.
“Ningependa kuitimisha kwa kuwapongeza ATE kwa namna ambayo wamekwenda na mabadiliko ya kidijiti katika kuhudumia waajiri nchini, Mtendaji mkuu ametueleza namna ambavyo lango la waajiri (membership portal) litaweza kuboresha huduma kwa waajiri kwa kutumia mtandao,” amesema Katambi.
Leave a comment