May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Alichokisema Dk. Hoseah baada ya kushinda urais TLS

Spread the love

DAKTARI Edward Hoseah, Rais Mteule wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), amesema, uchaguzi wa nafasi hiyo ulikuwa na ushindani mkubwa na Watanzania, wana matarajio makubwa na chama hicho. Anaripoti Regina Mkonde, Arusha…(endelea).

Uchaguzi wa Urais wa TLS, umefanyika leo Ijumaa tarehe 16 Aprili 2021, katika viwanja vya kituo cha mikutano cha kimataifa cha Arusha (AICC), jijini Arusha.

Katika uchaguzi huo, Dk. Hoseah alichuana na Flaviana Charles, Shehzada Walli, Albert Msando na Francis Stolla.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi na Charles Rwechungura, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TLS, Dk. Hoseah amesema, wagombea wenzake walimpa ushindani mkubwa.

“Wagombea wenzangu mmetoa ushindani mkali sana. Uchaguzi haukuwa mwepesi, kwa mara ya kwanza umeenda viral sio tu TLS  bali kwa Tanzania nzima.”

“Hii inaonesha kiasi gani tasnia ya sheria ni muhimu katika maisha ya Watanzania. Watanzania wote wamekuwa wakifuatilia uchaguzi huu,” amesema Dk. Hoseah, aliyewahi kuwa mkutugenzi mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru).

Kuhusu uchaguzi huo, Dk. Hosea ameupongeza uongozi wa TLS kwa kuendesha uchaguzi katika misingi ya uhuru na haki.

“Watanzania watengemee chama chenye uwazi, kitawajibika kuwatetea  bila kujali rangi, sura wala kabila. Ni kazi yetu kuwatetea Watanzania, tutahakikisha tunasimamia na kuishauri serikali. naimani serikali iliyoko madarakani ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu,” amesema Dk. Hoseah

Akizungumzia utendaji kazi, Dk. Hoseah amesema,”Tutaendelea kushauri Serikali na mamlaka zake zinazohusika, sisi ni waungwana, hatutatumia lugha ya mapambano, lugha yetu ni utu. Ili usikilizwe na mkubwa lazima uongee kwa utu, usipoongea kwa utu, mkubwa hatokusikiliza. Najua serikali inavyofanya kazi.”

Dk. Hoseah ameshinda kwa kura 293, kati ya  kura 802 zilizopigwa na mawakili waliojitokeza.

Katika kinyang’anyiro hicho, Dk. Hoseah alichuana vikali na Flaviana Charles aliyepata kura 223, huku aliyeshika nafasi ya tatu ni Shehzada akipata 192.

Aliyeshika nafasi ya nne ni  Msando aliyepata kura 69 na wa mwisho, Stolla alipata kura 17.

Dk. Hoseah anarithi mikoba ya Dk. Ruegemeleza Nshala, aliyemaliza muda wake.

Kwa mujibu wa sheria ya TLS, Dk. Hoseah ataongoza katika kipindi cha mwaka mmoja (Aprili 2021 hadi Aprili 2022).

error: Content is protected !!