Saturday , 4 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Barua ya Lissu yatua Kisutu
Habari MchanganyikoTangulizi

Barua ya Lissu yatua Kisutu

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema
Spread the love

TUNDU Lissu, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameiandikia barua Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kueleza amelazimika kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya kuangaliwa afya yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa ya kuwepo kwa barua ya Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema na pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, imepatikana leo tarehe 3 Desemba 2020, wakati wa kuendelea kwa kesi ya madai ya uchochezi inayomhusu pamoja na waliokuwa watendaji wa Gazeti la Mawio.

Taarifa za kimahakama zinaonesha kuwa, Lissu amemwandikia barua rasmi Hakimu Mkazi Mwandamizi Thomas Simba, anayesikiliza kesi hiyo.

Kwenye barua hiyo, Lissu ameeleza kwamba, amelazimika kuondoka nchini kwenda Ubelgiji ambako amekuwa akitibiwa tangu alipokutwa na mkasa wa kushambuliwa kwa risasi kadhaa akiwa jijini Dodoma kwa shughuli za Bunge.

Lissu alikuwa mbunge wa Singida Mashariki alipopigwa risasi tarehe 7 Septemba 2017, wakati akiwasili eneo la makazi yake la Area D, Dodoma, mchana siku hiyo akitokea kwenye ukumbi wa Bunge.

Alikimbizwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma alikopatiwa matibabu ya huduma ya kwanza, baadaye kusafirishwa kupelekwa nchini Kenya ambako alilazwa Hospitali Kuu ya Nairobi.

Miezi miwili baadaye, alipelekwa nchini Ubelgiji ambako alifanyiwa upasuaji mara 21 ikiwemo kutolewa risasi mwilini. Alirejea nchini Agosti mwaka huu na kushiriki uchaguzi mkuu akiwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu

Mbele ya Mahakama ya Kisutu leo, pale Hakimu Simba alipoita mshitakiwa wa nne, Lissu, alitokea Robert Katula, mmoja wa wadhamini wake wawili, na kueleza kuwa mshitakiwa “anaumwa na amesafiri nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu.”

Mbali na Lissu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo iliyofunguliwa Juni 2016, ni Jabir Idrissa aliyekuwa mwandishi wa Mawio, Simon Martha Mkina (Mhariri) na Ismail Mehboob aliyekuwa meneja wa mtambo uliochapa gazeti.

Mwanahalisi Online imefahamu zaidi kuwa, Lissu aliandika barua ambayo mahakama iliipokea tarehe 13 Novemba 2020 na kujumuishwa kwenye jalada la kesi, kwa upande wa mashitaka pamoja na mawakili husika.

Lissu alikuwa akijitetea mwenyewe mahakamani kwa muda wote kesi ilipokuwa ikisikilizwa. Tayari upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi wawili kutoa ushahidi kabla ya Lissu kushambuliwa kwa risasi na kesi hiyo kulazimika kutoendelea kutolewa ushahidi.

Kutoka hapo, kesi hiyo imekuwa ikiitwa na kupangiwa siku nyingine na kukawa na wakati wadhamini wa Lissu wakibanwa na mahakama kumleta mshitakiwa. Katika kutafuta njia ya kujinusuru na adhabu ya mahakama, wadhamini tayari waliwasilisha ombi la kutaka mahakama itoe hati ya kumkamata Lissu.

Ombi hilo limepengwa kutolewa uamuzi tarehe 21 Januari 2021, siku ambayo pia hakimu amepanga kesi iendelee kusikilizwa.

Kesi hiyo iliibuliwa na Jamhuri baada ya gazeti la Mawio kuchapisha habari iliyobebwa na maneno “Maafa yaja Zbar” iliyotokana na mahojiano na Lissu kuhusu ushauri wake kwa kadhia ya kufutwa kinyemela uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015.

kwenye andiko hilo, Lissu alimshauri Rais Dk. John Magufuli kumaliza mgogoro ulioibuka kufuatia tamko la Jecha Salim Jecha, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kwa kuingilia kati na kuamuru kurudishwa haki ya ushindi wa uchaguzi kwa Maalim Seif Sharif Hamad akidai aliongoza kwa kura akiwa mgombea kupitia Chama cha Wananchi (CUF).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

RPC Dodoma akabidhiwa bunduki mbili za wahalifu

Spread the love  Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yazindua huduma maalum kwa wastaafu

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua huduma maalum kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yazindua akaunti ya Kikundi

Spread the loveBenki ya NMB imezindua akaunti ya kikundi yenye  maboresho makubwa...

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

error: Content is protected !!