MRISHO Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini anapiga yowe kwamba, anahujumiwa na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Chama Chama Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha…(endelea).

Gambo aliyevurugana na Godbless Lema, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), analalamika kupata upinzani kutoka kwa viongozi wa serikali jijini humo.

Kama ambavyo Lema alivyokuwa akilalamikia kuhujumiwa wakati Gambo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, mbunge huyo wa sasa anatoa malalamiko ya namna ile ile kuhusu kuhujumiwa.

Lema na familia yake kwa sasa wanaishi ukimbizini nchini Canada, ni baada ya kukimbia Tanzania akidai, anatishiwa maisha yake. Amechukua hatua hiyo muda mfupi baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, na kumtangaza Dk. John Magufuli kuwa mshindi huku Jimbo la Arusha Mjini akitangazwa Gambo.

Godbless Lema

Gambo anasema, amekuwa akipigwa vita kabla ya uchaguzi mkuu, wakati wa uchaguzi mkuu na sasa baada ya uchaguzi mkuu huku akisisitiza, ‘hayupo wa kunizuia kufanya kazi hapa na hajazaliwa.’

Akizungumza na wananchama wa chama hicho jijini humo, Gambe amesema, alikuwa anapambana na wapinzani na sasa anapambana na viongozi wa serikali wanaotaka kumkwamisha.

Katika maelezo yake mbele ya wanachama wenzake, Gambo hakueleza kiini cha vita vyake na baadhi ya viongozi wa serikali ambao hakuwataja kwa majina wala vyeo.

“…sintakuwa tayari kumsikiliza mtu yeyote ambaye atataka kunikwamisha na kuhangaika na shida za watu, maana kuna wengine wanatangaza watamuweka mbunge ndani, mie?

“Unamuweka mbunge ndani kwa kipi? Na kwa sababu gani? Bado vita iko. Zamani tulikuwa tunapigana vita na wapinzani, sasa hivi tunapigana vita na viongozi wenzetu ambao lengo lao ni kuhakikisha mbunge wa jimbo hafanyi kazi yoyote,” amesema Gambo.

Amesema, miongoni mwa viongozi wa wilaya na mkoa wamekuwa wakiwakataza wataalamu kuongozana naye, hata hivyo amewashukuru wataalamu hao kuungana naye.

“Wako baadhi ya wataalamu kutoka Jiji la Arusha, kuna kipindi tulikuwa tunafanya ziara, tupo kwenye mkutano wa wananchi, mkurugenzi wa halmashauri anawapigia wataalamu waondoke kwenye mkutano wa mbunge ambaye anasikiliza kero za watu,” amesema Gambo.