July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali kukusanya, kutumia Tril 34.88 bajeti 2020/21

Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na MIpango Tanzania

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania, inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya Sh. 34.88 trilioni, katika Mwaka wa Fedha 2020/21. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi tarehe 11 Juni 2020 na Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, wakati akisoma mapendekezo ya serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021, bungeni jijini Dodoma.

Katika Makadirio na Mapato ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2019/20, serikali ilipanga kukusanya na kutumia Sh. 33.1 trilioni ambapo katika mwaka wa fedha 2018/19, serikali ilipanga kukusanya na kutumia Sh – 32.5 Trilioni

Kwa mujibu wa mapendekezo yaliyotolewa na Dk. Mpango leo, serikali inatarajia kukusanya mapato ya ndani Sh. 24.07 trilioni (asilimia 69.0 ya bajeti yote), kati ya mapato hayo, mapato ya kodi ni Sh. 20.33 trilioni na mapato yasiyo ya kodi Sh. 2.92 trilioni.

Serikali imepanga kukusanya Sh. 815 bilioni kutoka katika vyanzo vya mapato ya halmashauri.

Wakati huo huo, Serikali imepanga  kukopa Sh. 4.90 trilioni, kutoka soko la ndani ambapo Sh. 3.32 trilioni kati ya fedha hizo zitakazokopwa, ni kwa ajili ya kulipia hati fungani na dhamana za Serikali zinazoiva.

Na kiasi cha Sh. 1.59 trilioni , kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Sambamba na hilo, Serikali imepanga kukopa Sh. 3.04 trilioni kutoka katika soko la nje kwa masharti ya kibiashara , kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, Washirika wa Maendeleo wanatarajia kuchangia misaada na mikopo nafuu kiasi cha Sh. 2.87 trilioni (asilimia 8.2 ya bajeti).

“Kati ya kiasi hicho, miradi ya maendeleo ni shilingi trilioni 2.46; Mifuko ya Pamoja ya Kisekta shilingi bilioni 138.3; na Misaada na Mikopo nafuu ya Kibajeti (General Budget Support-GBS) shilingi bilioni 275.5,” inaeleza taarifa hiyo ya mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Katika matumizi ya fedha hizo za bajeti (Sh. 34.88 trilioni), Sh.  22.10 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida (asilimia 63 ya bajeti), ikiwemo Sh. 10.48 trilioni kwa ajili ya ulipaji wa deni la serikali, Sh. 7.76 trilioni kwa ajili ya mishahara na Sh. 3.74 matumizi mengineyo.

Pia, serikali imepanga kutumia Sh. 12.78 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ambayo ni sawa na asilimia 37 ya bajeti yote.

Matumizi hayo ni pamoja na kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge (2.10 trilioni), mradi wa kufua umeme Mto Rufiji (Sh. 1.60 Tril.), mifuko ya Reli (Sh. 823.7 Bil.), Maji na REA (Sh. 490 Bil).

“Sh.  490 Bil.  ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, na Sh. 298.1 Bil. kwa ajili ya elimu msingi bila ada. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 600.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, watoa huduma na makandarasi wa barabara, maji na umeme,” inaeleza taarifa ya mapendekezo hayo.

error: Content is protected !!