January 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Mwinyi awasimamisha kazi vigogo Wizara ya Fedha

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

Spread the love

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi amemsimamisha kazi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii visiwani humo(ZSSF), Sabra Issa Machano na watendaji wa Kamati  ya Uratibu wa Mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) kutoka Wizara ya Fedha, ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea).

Rais Mwinyi amewasimamisha kazi watendaji hao leo Jumatano tarehe 23 Desemba 2020, wakati anazungumza na watendaji wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), katika ukumbi wa taasisi hiyo uliopo Victoria Garden,  Vuga visiwani humo.

Machano na vigogo hao wa Wizara ya Fedha wanakabiliwa na tuhuma za ukiukwaji wa taratibu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar,  amesema Machano na wenzake akiwemo Ramadhani Andalla Ali, walifanya makosa ya kiutendaji katika utekelezaji wa mradi wa jumba la treni lililopo Darajani visiwani humo.

Rais Mwinyi amesema taarifa zilizopo zinaonyesha makosa makubwa katika manunuzi pamoja na kufanyika udanganyifu juu ya kazi zilizoelezwa kufanyika, katika mradi huo.

Kufuatia makosa hayo, Rais Mwinyi ameagiza mamlaka husika kufanya uchunguzi wakati wahusika wakiwa nje ya ofisi zao baada ya kusimamishwa kazi.

Wakati huo huo, Rais Mwinyi ameagiza ZAECA kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya Mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  Haidar Mussa Maisara  anayetuhumiwa kushusha kiwango cha kodi  katika tukio la kuingizwa Bandarini kichwa cha Scania.

Sambamba na Kampuni ya KEVIS aliyoagiza ifanyiwe uchunguzi.

Rais Mwinyi amemtuhumu mfanyakazi huyo kujihusisha na vitendo vya rushwa mara kwa mara, kwa kushusha kiwango cha kodi tofauti na kiwango kilichopangwa kwa mujibu wa sheria.

Rais Mwinyi amesema tangu Serikali ya Awamu ya nane iingie madarakani, imebaini kuwepo matatizo makubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, na kuahidi kudhibiti mianya ya rushwa na idanganyifu katika miradi hiyo.

Rais Mwinyi amesema tangu Serikali ya Awamu ya nane iingie madarakani, imebaini kuwepo matatizo makubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa, na kiahidi kudhibiti mianya ya rushwa na idanganyifu katika miradi hiyo.

Waziri wa Nchi (OR) Katiba, sheria, utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman ameahidi kutokomeza vitendo vya rushwa kwa kutumia ZAECA na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU).

Naye, Mkurugenzi Mkuu ZAECA Mussa Haji Ali, amesema taasisi hiyo inaendelea kufanya uchunguzi katika miradi mbali mbali ikiwemo wa Ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri na  ukarabati wa jengo la Treni ambayo imebainika kuwepo vitendo vya  rushwa.

Alisema miradi mingine inayoendelea kufanyiwa uchunguzi ni Barabara ya Bububu  – Mkokotoni Kaskazini Unguja pamoja na ile ya Ole – Kengeja inayoonekana kuwepo harufu ya rushwa katika suala la tathmini.

Aidha, aliitaja miradi mingine inayoendelea kufanyiwa uchunguzi kwa tuhma za kuwepo mianya ya rushwa, kuwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Amali Vitongoji, Bandari ya Mangapwani, Soko la Matunda Kangani, Ujenzi wa kiwanda cha ushoni  cha Idara Maalumu.

Na mradi wa kuendeleza vijana, ujenzi wa vituo vya zimamoto Pemba, Kuimarisha majengo ya JKU Mtoni, Matengenezo kambi ya KVZ Pemba pamoja  Chuo cha Mafunzo Wete.

error: Content is protected !!