January 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli ahofia udukuzi nyaraka za Serikali

Rais John Magufuli

Spread the love

RAIS wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kutoendesha shughuli zake kwa njia ya mtandao, ili kudhibiti uvujaji wa taarifa za watumishi wa umma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Kiongozi huyo wa Tanzania ametoa agizo hilo leo Alhamisi tarehe 24 Desemba 2020, wakati anamuapisha Jaji wa Mahakama ya Rufani, Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi, kuwa Kamishna wa Maadili, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Jaji Mwengesi aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Kamishana wa Maadili jana tarehe 23 Desemba 2020, ambapo anachukua nafasi ya aliyekuwa Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Haroid Nsekela aliyefariki dunia tarehe 19 Desemba 2020.

“Kwa mfano Chief Secretary (Katibu Kiongozi), fomu yake mle aeleze alichonacho, na labda hata awe na nyumba ndogo, aseme nina nyumba ndogo ambayo sijaitangaza kwa mke wangu halafu aweke kwenye mtandao, halafu mtu awe anaijua ile password (Nywila),  ule usiri na utakatifu wa idara hiyo mnaupoteza,” amesisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, katika zama hizi kuna wadukuzi wengi, hivyo ni hatari watumishi wa umma kuweka taarifa zao mitandaoni.

“Hatutakiwi kuwa opened in that way (wawazi),  lazima pawe na usiri wa fomu hizi (fomu zao za matamko ya mali na madeni) , mtu akishajua program anaweza aka-edit (hariri). Ma – Hackers (wadukuzi) wako wengi, umejaza una Mil. 10 atakujazia Mil. 100. Baadae unakuja kuulizwa ulijaza Mil. 100, saini yako hii hapa,” amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo, Rais Magufuli amesema fomu zinazofanyiwa skani kwa ajili ya kuwekwa mtandaoni, zinapoteza  uhalisia wake.

Rais Magufuli amewashauri watumishi wa umma baada ya kupakua fomu hizo kutoka katika mtandao wa sekretarieti hiyo, wazijaze na kuzirudisha kwa njia ya kawaida, katika mamlaka husika.

“Fomu zenu mlikuwa mnatoa kwa mtandao na mlisema baadhi ya hizo fomu ziwe zinarudhishwa kwa mtandao, unaweza ukafanya mambo mengine yote kwa njia ya mtandao, lakini ajaze fomu arudishe katika maeneo yao,” amesema Rais Magufuli.

Amemuelekeza Jaji Mwengesi kwa kushirikiana na watumishi wake, kulifanyia kazi suala hilo.

“Ni vyema waka download (pakua)hizo fomu zenu, lakini wanaporudisha warudishe mahali zinapotakiwa. Wao wenyewe badala ya kuzi-Scan na kuzileta mtandaoni.  Ninajua wasaidizi wako watakuwa wamenielewa,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa, maelekezo hayo yalishawahi kutolewa kwa watumishi wa sekretarieti hiyo na marehemu Jaji Nsekela alipokuwa Kamishna wa Maadili.

“Nilimueleza marehemu Jaji Nsekela na tulikuwa tunakubaliana kwamba fomu unaweza download (pakua) kwenye mtandao lakini ukijaza na kurudisha,  usizirudihe kwa kufanya scaning na kuzirudisha tena kwenye mtandao,” amesema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amewaagiza watumishi wa umma, kuwasilisha fomu zao za matamko ya mali na madeni katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kabla ya tarehe 30 Desemba 2020 ili zifanyiwe kazi.

“Na niwaombe wafanyakazi wenzangu ambao wanatakiwa kujaza fomu,  wahakikishe wanajaza kabla ya tarehe 30 Desemba 2020, ili zimfikie kamishna mpya kwa sababu sasa hakuna sababu tena ya kisingizio.

Najua wengi ninapozungumza hapa hawajapeleka fomu zao, hata mimi yangu nilikuwa bado sijapeleka. Sasa nitaijaza harakaharaka ili niweze kukufikishia hizo fomu kwa taratibu na sheria zetu,” amesema Rais Magufuli.

error: Content is protected !!