Wednesday , 29 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Jecha aibuka, amtuhumu Maalim Seif kuiba kura
Habari za Siasa

Jecha aibuka, amtuhumu Maalim Seif kuiba kura

Maalim Seif Sharrif Hamad, Mgombea Urais Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo
Spread the love

JECHA Salim Jecha, aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ameibuka upya. Safari hii anasema, aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Maalim Seif Sharif Hamad, aliiba kura. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Katika mahojiano yake na gazeti la kila wiki la Raia Mwema, Jecha anasema, ZEC iligundua kuwapo kwa wizi wa kura uliofanywa na Maalim Seif na chama chake – The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi), na kwamba hatua hiyo, ndiyo iliyomsukuma yeye kufuta uchaguzi.

“…nilipojumlisha kura zote zilizopigwa, niligundua kuwa kuna kura 15,000 (elfu kumi na tano) zikiwa zimeongezeka. Kura hizi, ni nje ya idadi ya kura tulizochapisha kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.”

Kwa mujibu wa Jecha, lingine lililomsukuma kufuta uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na matokeo yake, ni hatua ya Maalim Seif, kujitangaza mshindi, kinyume na sheria za uchaguzi.

Hata hivyo, Maalim Seif amekana madai hayo kwa kusema, “nadhani Jecha amezeeka au amekunywa maji mengi ya bendera na hivyo yamemlevya. Mimi sijawahi kuiba kura. Sijawahi kufanya udanganyifu, kwa kuwa naamini katika uchaguzi wenye ushindani na kidemokrasia.”

Kabla ya Jecha kutangaza kufuta uchaguzi huo na matokeo yake yote, tayari uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW), ulikuwa umefanyika na washindi kukabidhiwa vyeti.

Aidha, kabla ya Jecha kutangaza kufutwa kwa uchaguzi, kituo kikuu cha kutangazia matokeo kilichokuwepo Hoteli ya Bwawani, kilizingirwa na vikosi vya jeshi na polisi.

Vilevile, wakati Jecha akifanya maamuzi hayo, ripoti za waangalizi zilizoonyesha uchaguzi wa 25 Oktoba, Visiwani ulikuwa huru, ni pamoja na ile iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya (SADEC), pamoja na Umoja wa Africa (AU).

Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi – Zanzibar na Muungano – pale matokeo ya mbunge, mwakilishi; na au diwani, yanapotangazwa na mshindi kukabidhiwa cheti chake, basi mamlaka ya kubatilisha chochote, yanabaki mikononi mwa mahakama.

Katika ripoti yake, waangalizi wanasema, wameridhika na zoezi zima la uchaguzi wa 25 Oktoba 2015, upigaji kura, kuhesabu na kujumuisha matokeo.

Alipoulizwa Maalim amewezaje kupata kura za ziada wakati ZEC ilichapisha kura zake, nchini Afrika Kusini, Jecha anasema, “mimi sijui namna walivyozipata. Wala sikuwaona, ila inasemekana walienda Afrika Kusini katika kampuni ile tulikochapa kura, wakaja na masanduku yenye karatasi za kupigia kura.”

Huku Jecha akidai kuwa alikuwa na mamlaka ya kufuta uchaguzi, Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa, alipinga maamuzi ya mwenyekiti wake akisema hana mamlaka hayo na hivyo, kuamua kuendelea na kazi ya majumuisho ya kura katika hoteli ya Bwawani, lakini alikamatwa na kushikiliwa kwa saa nne makao makuu ya polisi ya Zanzibar, katika eneo la Kilimani, Unguja.

Alichukua uamuzi huo, huku kura zikiwa zimeshahesabiwa katika majimbo karibu yote ya uchaguzi na washindi wameshatangazwa; huku wengine wakiwa wamekabidhiwa vyeti vya ushindi.

Katika Uchaguzi mkuu uliyopita, Jecha Salim Jecha, aliushangaza ulimwengu, kufuatia hatua yake ya kuamua kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kuteuliwa na Chama Chama Mapinduzi (CCM), kuwania urais wa Zanzibar.

Hatua ya Jecha kujitosa katika kinyang’anyiro hicho cha urais, ilithibitisha madai ya baadhi ya Chama vya upinzani, kwanba uamuzi wake wa kufuta uchaguzi ulilenga maslahi binafsi ya chama chake hicho alichotaka kumpitisha kuwania nafasi hiyo.

Kwa taarifa zaidi, soma gazeti la Raia Mwema, toleo la leo, Jumatano – Mhariri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!