MAXENCE Melo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Jamii Forums, amehukumiwa kutotenda kosa la kuzuia Jeshi la Polisi kutekeleza wajibu wao kwa mwaka mmoja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Hukumu hiyo imetolewa leo tarehe 17 Novemba 2020 na Huruma Shaidi, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam baada ya kumkuta na hatia katika shitaka lake la kuzuia upelelezi wa Jeshi la Polisi.
Wakati akitoa hukumu ya kesi hiyo namba 458 ya mwaka 2016, iliyokuwa inamkabili Melo na mwenzake Mike Mushi, Huruma Shaidi amesema mahakama imemuacha huru Melo kwa masharti ya kutofanya kosa kama hilo ndani ya mwaka mmoja. Mushi hakukutwa na hatia yoyote.
Katika kesi hiyo, Melo na Mushi walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili, kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa kwa kikoa cha Tanzania (.Tz) na kuzuia upelelezi wa Jeshi la Polisi.
Ambapo, Melo alikutwa na hatia katika shitaka la kuzuia Upelelezi wa Jeshi la Polisi huku mwenzake akikutwa hana hatia katika mashtaka yote mawili.
Katika kesi hiyo, Melo alikuwa akituhumiwa kutotoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu wanachama wawili wa Jamii Forums waliodaiwa kuandika madai ya uhalifu uliotuhumiwa kufanywa na benki ya CRDB kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Leave a comment