Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kubenea kuingia na hoja ya watu wenye Ualbino bungeni
Habari za Siasa

Kubenea kuingia na hoja ya watu wenye Ualbino bungeni

Spread the love

MBUNGE wa Ubungo (CHADEMA), Saed Kubenea, amepanga kuwasilisha hoja binasfi bungeni, kushinikiza serikali kuridhia Itifaki ya pamoja ya Mkataba wa Afrika wa haki za binadamu, kuhusu haki za watu wenye Ualbino nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Jumapili, tarehe 11 Agosti 2019, jijini Dar es Salaam, Kubenea amesema, mkataba huo uliyopitishwa katika mkutano wa 30 wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika mwaka jana, una umuhimu mkubwa kwa taifa ili kulinda jamii hiyo.

Aidha, mbali na kutaka kuridhiwa kwa mkataba huo, Kubenea amesema, atatumia hoja hiyo, kuitaka serikali ku fanyia marejeo sera ya watu wenye ulemavu inayotumika sasa, ili iweze kukidhi mahitaji ya makundi yote ya watu wenye ulemavu.

“Jamii ya watu wenye Ualbino, ipo hatarini kufutika kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kushamiri kwa imani za kishirikina. Hivyo basi, ni wajibu wetu kama taifa, kuilinda jamii hii na kuihakikishia usalama wa maisha yao,” ameeleza.

Amesema, hatua ya serikali ya kuridhia Itifaki ya mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu kuhusu haki za watu wenye Ualbino, itakuwa inatambua na kuvisemea vitendo hivyo vya mauaji na ukatwaji viungo kwa watu wenye ualbino barani Afrika pamoja na kufafanua maana ya mauaji ya kishirikina.

Ameongeza, “hakikisho hilo, haliwezi kupatikana kwa njia ya matamko ya kwenye majukwaa. Tunataka haki hizo, zitajwe kwenye sera na miongozo mbalimbali.”

Kubene amesema, mbali na jamii hiyo kuuliwa kwa imani za kishirikina, hukumbana pia na tatizo kubwa la saratani ya ngozi, uoni hafifu, kukatwa viungo, pamoja na kufukuliwa kwa makaburi yao.

Amesema, “tunataka kujengwa mfumo thabiti na madhubuti wa kisera, kisheria, kiuongozi, kitaasisi, na kibajeti ili kukomesha ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu, ingawa Itifaki hii bado haijaridhiwa na kusainiwa na nchi yetu.”

Anasema, itifaki hiyo na maboresho ya sera ya watu wenye ulemavu, anapendekeza yafanyike ndani ya kipindi hiki cha uhai wa Bunge hili la Kumi na Moja (11).

Kwa mujibu wa Kubenea, Sera ya Watu wenye ulemavu ilitungwa mwaka 2004 ili kuweza kusaidia kukomeshwa vitendo vya kikatili dhidi ya jamii hiyo.

Ameyashukuru mashurika na taasisi zote zinazohudumia watu wenye Ualbino, wakiwamo Chama cha wenye Albino nchini (TAS) na taasisi mashuhuri inayotetea watu wenye ualbino ya Under The Same Sun (UTSS), kutokana na mchango wao mkubwa kwake katika kufanikisha hoja hiyo.

Naye Mwanasheria kutoka UTSS, William Maduu amesema, Kubenea anahitaji kuungwa mkono. Amesema, “amefanya jambo kubwa na zuri. Ni vema tukamuunga mkono na kila mtu anayeguswa na madhira ambayo watu wetu wanapitia, basi tunamuomba kwa mikono miwili, asaidie hoja hii iingie bungeni na ipite.”

Maduu amesema, Afrika ndio bara pekee ambalo watu wake wanaamini ili wawe tajiri lazima apate kiungo au nywele ya mtu mwenye ualbino. Hivyo, “tunamshukuru mheshimiwa Kubenea kwa nia ya kutaka kututoa huko.”

Akizungumzia itifaki hiyo ya Afrika, Maduu alisema, mkataba huo wa kimataifa unapinga jambo hilo kwa nguvu zote hivyo ni muhimu kwa Serikali kuweza kuuridhia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha watu wenye Ualbino jimbo la Ubungo, Mussa Geuza alisema, anawaomba wabunge wengine waungane na Kubenea katika kuwatetea na kuhakikisha mkataba huo Serikali inaweza kuuridhia.

Itifaki ya pamoja ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu kuhusu Haki za Watu Wenye Ualbino ulipitishwa mjini Addis-Ababa Ethiopia, tarehe 29 Januari 2018, wakati wa mkutano wa 30 wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika.

Kubenea anasema, hatua ya serikali ya kuridhia Itifaki hiyo, kutasaidia kuthibitisha kwa vitendo, kwamba taifa letu lina dhamira njema ya kudumisha haki na ustawi wa watu wenye ualbino; na kutaifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa na jumuiya ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.

Katika hatua nyingine, Kubenea amesema, uamuzi wake wa kupeleka hoja hiyo bungeni, ni kumuenzi aliyekuwa mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kutokana na mchango wake kwa watu wenye Ualbino.

“Kuna mambo ambayo Dk. Mengi aliyasimamia. Miongoni mwao, ni pamoja na hili. Hivyo basi, mimi kama mmoja wa vijana ambao tumelelewa na Dk. Mengi, nimeamua kupeleka hoja hii bungeni, kwa lengo la kumuenzi,” ameeleza.

Amesema, “ninaowamba wale wote ambao walikuwa marafiki wa Mengi na waliokuwa wanathamini mchango wake, kuniunga mkono kwa heshima ya mzee wetu huyu aliyefariki dunia miezi mitatu iliyopita.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!