Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kinana, Makamba watakiwa kufukuzwa CCM 
Habari za SiasaTangulizi

Kinana, Makamba watakiwa kufukuzwa CCM 

Spread the love

JOSEPH Msukuma, mbunge wa Geita Vijijini, amewatuhumu makatibu wakuu wawili wastaafu wa chama Chama Cha Mapinuduzi, Kanal Abdulrahaman Kinana na Luteni Yusuf Makamba, kuwa wanataka kukivuruga chama chao. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, mkoani Geita, Msukuma amesema, yeyote anayempinga Rais Magufuli ili kumzuia asimalize mihula yake miwili ya uongozi kwa mujibu wa taratibu za CCM, atakuwa anajichimbia kaburi.

Amedai kuwa kitendo kilichofanywa na Kinana na Makamba, ni hujuma, uasi na usaliti dhidi ya rais Magufuli, ni kwamba ni wajibu wa chama hicho, kuwashughulikia haraka kwa mujibu wa taratibu zake.

“Kilichofanywa au kinachofanywa na wastaafu hawa wakiwemo baadhi ya mawaziri kwenye serikali yako na wabunge ndani ya chama chako, kuthubutu kukupinga kwa siri na waziwazi, ni uasi na sharti uzimwe sasa,” ameeleza Msukuma.

Kinana na Makamba, wameripotiwa kumwandikia barua Katibu wa Baraza la Ushauri la viongozi wakuu wastaafu wa CCM, Pius Msekwa, kulalamika kufachuliwa majina, kudhalilishwa na kutungiwa uongo na Cryspian Musiba.

Aidha, Kinana na Makamba, wamenukuliwa kupitia taarifa yao kwa umma, wakimtuhumu Musiba kuvuruga nchi na kuhatarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Musiba amekuwa akitumia magazeti yake na mitandao mingine ya kijamii, kushambulia watu mbalimbali, huku akijitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Rais John Magufuli.

Katika waraka wao waliosambaza kwenye vyombo vya habari na ambao umepewa kichwa cha maneno kisemacho, “taarifa kwa umma,” viongozi hao wawili wamehoji sababu za vyombo vya dola, kunyamazia matamshi ya Musiba.

Taarifa inaeleza na pia kuhoji, maswali kadhaa, ikiwamo, “huyu mtu (Musiba), bila shaka atakuwa anakingiwa kifua na baadhi watu wakubwa ndani ya serikali. Lakini tunajiuliza, anakingiwa kifua kwa maslahi ya nani? Anatumika kwa malengo gani? Nini hatima ya mikakati yote hii?”

Kwa mujibu wa Kanal Kinana na Luteni Makamba, tafakari yao inaonyesha kuwapo ushahidi wa kimazingira, kwamba “mtu huyu (Musiba), anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala mtu yeyote.”

Wanasema, “zipo ishara kuwa watu wanaomkingia kifua Musiba, wana mamlaka, baraka na kinga, ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalumu kwa watu maalumu na kwa malengo maovu.”

Kanal Kinana na Luteni Makamba wanasema, “mtu huyo anatumika kwa malengo ya kuwazushia, kuwakejeli, kuwavunjia heshima, kuwatia hofu na kuwanyamazisha viongozi, taasisi na watu ambao ni walengwa waliokusudiwa.

“Kuna kila dalili, kwamba lengo na hatima ya mkakati huu, ni kuandaa tufani ya kuwahusisha walengwa, wastaafu na walio kazini katika nafasi mbalimbali na matendo ya kihalifu, kimaadili na kihaini ili kuhalalisha hayo wanayokusudia kuyafanya.”

Msukuma ametaka watu hao aliowaita, “wasaliti wakubwa,” kuadhibiwa, kama ambayo imefanyika kwa baadhi ya viongozi waliotaka kuunda uasi kwa ajili ya kuvunja Muungano wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.

“Kama ilivyokuwa kipindi cha utawala wa Mwl. Julius Nyerere, ambapo Rais wa Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, aliandaa usasi wa kuvunja Muungano, na baadaye katibu mkuu wa CCM, Horace Kolimba kudai CCM kimepoteza dira, hatua kama hizo zinapaswa kuchukuliwa kwa Kinana, Makamba na wenzake wengine.”

Anasema, “kipimo chako (Rais Magufuli), cha ukomavu kisiasa na kiutawala, ni jinsi utakavyoweza kuhimili misukosuko ya kisiasa kwa kukabiliana na uasi na usaliti ndani ya chama; na uasi na usaliti ndani ya serikali, kama ilivyo kwa wapinzani.”

Msukuma ni mmoja wa wabunge wa Kanda ya Ziwa Victoria, wanaonekana kuwa na ushawishi mkubwa kwa Rais Magufuli, hadi kufikia hatua kwa baadhi ya wachambuzi kusema, kauli ya mbunge huyo, yaweza kuwa ndio mtazamo wa rais.”
 
Hata hivyo, Msukuma ameshindwa kujibu madai ya Kinana na Makamba, kuwa wanachokijadili siyo uasi, uhaini wala usaliti. 

Katika waraka wao, Makamba na Kinana wanasema, wameamua kutochukua hatua za kisheria, angau kwa sasa, kwa sababu kwanza jambo hili lina taswira ya kimkakati na lina mtandao wenye malengo ya kisiasa. Kwa hiyo linapaswa kushughulikiwa kisiasa.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!