Friday , 26 April 2024
Home Habari Mchanganyiko TMA wataja sababu za ongezeko la joto nchini
Habari Mchanganyiko

TMA wataja sababu za ongezeko la joto nchini

Joyce Makwata, Mtaalam wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)
Spread the love

 

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa juu ya uwepo wa ongezeko la joto katika maeneo mbalimbali nchini huku ikieleza sababu zinazosababisha hali hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na TMA leo tarehe 17 Novemba, 2022 imeeleza kuwa hali hii imesababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo mengi hapa nchini kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). Jua la utosi huambatana na hali ya ongezeko la joto kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine.

Katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2022, hali ya joto iliongezeka katika maeneo mbalimbali nchini. Kiwango cha juu zaidi cha joto cha nyuzi joto 36.9 0C kiliripotiwa katika kituo cha Mpanda, Katavi mnamo tarehe 26 Oktoba, 2022. Kiwango hiki ni sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.0 0C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Oktoba.

Aidha, baadhi ya maeneo mengine yaliyokuwa na ongezeko la joto kwa mwezi Oktoba, 2022 ni pamoja na mkoa wa Tabora nyuzi joto 35.7 (ongezeko la nyuzi joto 3.0), Moshi nyuzi joto 34.1 (ongezeko la nyuzi joto 3.2) na Dar es Salaam nyuzi joto 32.8 (ongezeko la nyuzi joto 1.4).

Hata hivyo, katika wiki mbili za mwanzo za mwezi Novemba, 2022; hali ya ongezeko la joto iliendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo ambapo kituo cha Mpanda kiliripoti nyuzi joto 35.4 0C mnamo tarehe 2 Novemba, 2022 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 4.7 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba. Kituo cha Tabora kiliripoti nyuzi joto 34.8 (ongezeko la nyuzi joto 3.7), Dar es Salaam nyuzi joto 33.7 (ongezeko la nyuzi joto 2.1) pamoja na Kilimanjaro nyuzi joto 34.3 (ongezeko la nyuzi joto 2.4).

Vipindi vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi Novemba, 2022 hususan katika maeneo yanayotarajiwa kuendelea kuwa na upungufu wa mvua na kupungua kidogo ifikapo mwezi Disemba, 2022 ambapo ongezeko la mtawanyiko wa mvua unatarajiwa.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kutoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za mwenendo wa hali ya hewa zinazotolewa pamoja na kutafuta, kupata na kutumia ushauri wa wataalamu wa kisekta ili kuepuka au kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa ikiwemo ongezeko la joto.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!