Mwenyekiti wa Kamati ya kufuatilia hali ya uchumi wa vyombo vya Habari, Tido Mhando amesema kutokana na mazingira magumu ya kisheria na kisiasa ambayo vyombo vya habari vimepitia katika Serikali ya awamu ya Tano iliyokuwa chini ya Rais John Magufuli, vyombo vingi vya habari vimejidhibiti kutoa habari za uwajibikaji kwa umma na kuhamia maudhui mepesi ya mzaha ‘comedy journalism.’ Anaripoti Faki Ubwa …(endelea).
Pia amesema vyombo hivyo sasa vimebeba maudhui ya burudani, mapenzi, muziki, michezo, tamthilia na vipindi vyenye tija ndogo kwa jamii.
Mhando ameeleza hayo leo Jumanne wakati akiwasilisha mapendekezo ya kamati yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mgeni rasmi kwenye kongamano la maendeleo ya sekta ya habari.
Mhando amesema aina hiyo ya uandishi inaleta madhara mawili makubwa, kwanza kudhoofisha uandishi unaozongatia uwajibikaji wa umma ambao ni muhimu kwenye jamii lakini pia kutengeneza kizazi kisochoweza kufikiria sawasawa kwa kuwa kinadumazwa na maudhui mepesi.
“Bila shaka sasa hivi tunaelewa kinachoendelea kuna kitu kinaitwa Comedy Journalism kumekuwa na mambo mengi ya mzaha mzaha yote haya yanatokana na wasiwasi waliokuwa nao waandishi, wamekuwa wanaogopa kutokana na mazingira magumu yaliyoletwa hapo mwanzo.
“Tunashukuru kwenye awamu yako hii ya sita yameanza kuondoka kidogo kidogo lakini kama ulivyotoa neno kwa viongozi hawa wa kisiasa wamekuwa wakileta ubabe ubabe katika sekta hii ya habari.
“Ubabe umekuwa mwingi tunaomba utasaidie kukabiliana na suala hili. Nina hakika hakuna chombo cha habari ambacho hakijatikiswa na ubabe huu kutoka kwa baadhi ya viongozi mifano ni mingi lakini nisingependa kuitaja hapa kwa sababu ya muda,” amesema.
Leave a comment