Friday , 3 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Wanaume Moshi hutandikwa na wake zao
Habari Mchanganyiko

Wanaume Moshi hutandikwa na wake zao

Spread the love

 

BAADHI ya wanaume, hususan walio ndani ya ndoa katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania, wamekuwa wakikumbana na vitendo vya kikatili, vikiwemo vipigo kutoka kwa wake zao, lakini hawasemi popote. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).

Imeelezwa wanaume hao huchapwa na wake zao kutokana na kukosa kipato huku wakikosa sehemu sahihi ya kufikisha malalamiko yao.

Kutokana na hali hiyo, wanaume hao kwa sasa wanakabiliwa na msongo wa mawazo ambapo wengine hufikia hatua ya kujiua au kutelekeza familia zao na kutokomea kusikojulikana ili kuondokana na vipigo ambavyo ni aibu kwenye jamii.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (TAPO), Manispaa ya Moshi, Rubelina Meena alisema vitendo vya ukatili kwa wanaume vinaendelea kushamiri siku hadi siku.

Alisema wanawake wanatumia udhaifu wa woga wa wanaume kusema vitendo hivyo kama njia ya kuvitekeleza.

“Wanaume wanatandikwa kisawasawa ndani ya nyumba na sisi wanawake na kwa kuwa tumeshajua ni waoga kusema basi hiyo ndio kama kinga yetu ila kiukweli vitendo hivi vipo na ni vya kukemea kwa gharama zozote zile,” alisema.

Kwa mujibu wa Rubelina, wanawake wengi kwa siku za hivi karibuni wameweza kujikwamua kiuchumi wakati hali ya kiuchumi kwa wanaume sio nzuri, jambo ambalo husababisha wanawake kubeba mzigo wote wa familia.

“Mama anarudi usiku saa tano, ameshakula na kunywa hajui hata mumewe amekula nini ila akiuliza tu mbona hakupikwi leo maneno ya masimango yanaanza na kupigwa sasa baba akiangalia mfukoni hana senti inabidi awe mvumilivu tu,” alisema

Alisema vitendo hivyo vimefanya baadhi ya wanaume kuzikimbia familia zao na kutokomea kusikojulikana ili kuficha aibu au kuepusha madhara ambayo yanaweza kujitokeza.

Kuhusiana na hali ya vitendo vya ukatili katika Manispaa ya Moshi, alisema bado vipo na kuwa bado jitihada mbalimbali zinaendelea kuhakikisha vitendo hivyo vinakwisha, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii.

“Hatuwezi kusema vitendo vya kikatili vimeisha kwani bado watu wapo tunachokifanya ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya vitendo hivi kwani athari zake ni nyingi lakini pia wadau nao waendelee kutuunga mkono,” alisema

Gregory Mmasy, mkazi wa Moshi alisema ni kweli wapo wanaume wanaopigwa na wake zao lakini jambo hili halionekani kama ni tatizo kwa sababu wanaume wanaona ni aibu kwenda kutoka taarifa kuwa kapigwa na mke wake na kuwa jamii itamchukuliaje.

“Hata ukienda pale Polisi (Dawati la Jinsia) sasa hivi ukisema umepigwa na mke watakuona kama ni mlevi ila mwanamke aseme tu kapigwa na mume, dakika hiyo hiyo ameshaenda kukamatwa sijui usawa hapa uko wapo?” alihoji.

Alisema kilichochangia kwa namna moja ama nyingine ni mtikisiko wa uchumi ambao umeonekana kuwakumba wanaume wengi na wakiwa hawana mbadala wa maisha tofauti na ilivyo kwa wanawake ambao wana njia nyingi ikiwemo vikoba na upatu.

“Unaweza kuachana na mwanaume mwenzako usiku akiwa mzima ila asubuhi ukikutana naye tayari ana ngeu ukimuuliza anasingizia ajali ya bodaboda ila ukweli ni kibano kweli tunatandikwa” alisema

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyakazi waidai STAMICO mishahara ya bilioni 1

Spread the loveWALIOKUWA wafanyakazi wa mgodi wa Shirika la Madini la Taifa...

AfyaHabari Mchanganyiko

200 wapimwa afya na GGML katika maonesho ya OSHA

Spread the loveZAIDI ya watu 200 jijini Arusha wamejitokeza kupimwa afya na...

Habari Mchanganyiko

Mfanyakazi CRDB atoa sababu za kubambikiwa kesi, hukumu Mei 30

Spread the love  MFANYAKAZI wa Benki ya CRDB, Ibrahim Masahi (40) ameieleza...

Habari Mchanganyiko

Waziri Ummy atangaza Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba

Spread the loveSERIKALI imesema imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha matibabu ya...

error: Content is protected !!