Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Bajeti 2020/21: ‘Blueprint’ kupangua ada, tozo 60 Tanzania
Habari za Siasa

Bajeti 2020/21: ‘Blueprint’ kupangua ada, tozo 60 Tanzania

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imependekeza kufuta au kupunguza ada na tozo 60 zinazotozwa na wizara, idara na taasisi zinazojitegemea ili kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa janga la homa kali ya mapafu (COVID-19) duniani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Hatua hizo ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa kuboresha Mfumo wa udhibiti wa Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment).

Hayo yamesemwa leo Alhamisi tarehe 11 Juni 2020 na Waziri wa Fedha na Mpango, Dk. Philip Mpango wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya 2020/21 bungeni jijini Dodoma.

Amesema, kufutwa kwa kodi hizo ni utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (Blueprint) kwa kurekebisha ada na tozo mbalimbali.

Mosi, Dk. Mpango amesema, Tume ya Ushindani, “napendekeza kufanya marekebisho ya kifungu cha 60 cha Sheria ya Ushindani kinachohusu adhabu ya makosa ya ushindani ili ihusishe tu pato ghafi lililopatikana ndani ya Tanzania Bara pekee na si duniani kote.”

“Lengo la mabadiliko haya ni kuifanya sheria hii itekelezeke kwa kuwa adhabu inayotokana na pato ghafi la kampuni za nje ni kubwa mno na hivyo kutolipika,” amesema

Pili, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Dk. Mpango amependekeza kufuta kipengele cha 16(2) cha Sheria ya makampuni ili kuondoa takwa la kugongewa muhuri na Kamishna wa Viapo ili kuonyesha umetimiza matakwa ya Sheria hiyo wakati unafungua kampuni au kuhuisha usajili. Aidha, Kifungu cha 14(4) kinatosheleza matakwa yote hayo na hivyo hatua hii itapunguza urasimu na gharama za kupata tamko la kutimiza matakwa ya kisheria (Declaration of Competence).

Tatu, Bodi ya Sukari. Dk. Mpango amependekeza kupunguza tozo inayotozwa na Bodi ya Sukari kutoka asilimia 2 ya thamani ya mzigo au asilimia 2 ya dola za Marekani 460 sawa na takriban dola za Marekani 9 kwa tani, chochote kitakachokuwa kikubwa hadi dola 7.5 kwa tani moja.

Nne, Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA). Dk. Mpango amependekeza kufuta tozo ya mafunzo ya elimu kwa umma iliyokuwa inatozwa kiasi cha Sh. 250,000 kwa kila mshiriki kwa kuwa hili ni jukumu la msingi la OSHA kuelimisha umma.

“Napendekeza kufuta ada ya ukaguzi iliyokuwa inatozwa kwa kiwango cha asilimia 80 ya ada ya usajili, ada hii inaleta mkanganyiko kwa kuwa tozo ya usajili ilishafutwa.”

“Napendekeza kupunguza ada ya uchunguzi wa ajali iliyokuwa ikitozwa kiasi cha Sh. 500,000 kwa kila mtaalamu anayefanya uchunguzi hadi Sh. 120,000 kwa kila mtaalamu lakini si zaidi ya Sh. 1 milioni,” amesema Dk. Mpango.

Tano, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Dk. Mpango amependekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Jeshi ya Zimamoto na Uokoaji Sura 427 kwa kupunguza ada na tozo zifuatazo:

(a) Kupunguza tozo ya Cheti cha Umahiri (Certificate of Competence) inayotozwa kwa wauzaji wa vifaa vya zimamoto na uokoaji kutoka Sh. 500,000 hadi Sh. 200,000.

(b) Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa usiozidi mita za mraba 2,000 kutoka Sh. 6 milioni hadi Sh. 100,000

(c) Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa kati ya mita za mraba 2001 hadi 4000 kutoka Sh. 6 milioni hadi Sh. 150,000.

(d) Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa kati ya mita za mraba 4001 hadi 9000 kutoka Sh. 6 milioni hadi Sh. 200,000

(e) Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye mitungi ya gesi yenye ujazo wa gesi kati ya tani 1 hadi tani 10 kutoka Sh. 2 milioni hadi Sh. 1,500,000

(f) Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maduka yanayouza mitungi ya gesi yasiyozidi ukubwa wa mita za mraba 100 kutoka Sh. 100,000 hadi Sh. 40,000

(g) Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maduka ya rejareja na maduka ya jumla kutoka Sh. 40,000 hadi Sh. 20,000

(h)  Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye vituo vidogo vya kuzalisha na kugawa umeme chini ya Megawatt 10 kutoka Sh. 6 milioni hadi Sh. 200,000

Dk. Mpango amependekeza pia kufanya marekebisho ya Sheria ya Jeshi ya Zimamoto na Uokoaji Sura 427, ili kuanzisha viwango vipya vya tozo kama ifuatavyo:

(a) Kutoza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto ya Sh. 2 milioni kwenye mitungi ya gesi yenye ujazo wa gesi kati ya tani 11 hadi tani 20; na

(b) Kutoza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kati ya Sh. 40,000 hadi Sh. 5 milioni kwenye taasisi ndogo za mikopo kutegemea na ukubwa wa eneo.

“Lengo la hatua hizi ni kuweka mazingira rafiki ya kibiashara na uwekezaji ili kuchochea uzingatiaji wa sheria kwa hiari na kuongeza wigo wa wadau wanautumia huduma za Jeshi la Zimamoto,” amesema Dk. Mpango

Sita, Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Dk. Mpango amependekeza kufanya marekebisho kwenye tozo mbalimbali kwenye Sekta ya Mifugo kama ifuatavyo:

(i) kufuta tozo ya kibali cha kusafirisha ngozi ndani na nje ya wilaya iliyokuwa ikitozwa Sh. 5000/=) kwa kibali; na

(ii) Kupunguza tozo mbalimbali kwenye sekta ya mifugo na mazao.

(iii) Kuongeza tozo mbalimbali kwenye sekta ya mifugo kama zilivyoainishwa ili kuhuisha tozo hizo kulingana na hali ya sasa ya thamani ya fedha;

(iv) Kuongeza ada ya kutunza mbuzi au kondoo kwenye vituo vya karantini, kupumzishia mifugo na ukaguzi kwa kila mmoja kutoka Sh. 200 hadi Sh. 500.

(v) Kutoza tozo mpya za vibali vya kusafirisha nje ya nchi na kuingiza ndani ya nchi mifugo na mazao yake.

(vi) Kutoza Sh. 20,000 kwa kibali cha kusafirisha pembe za ng’ombe, mbuzi na kondoo pamoja na kwato na mifupa ndani na nje ya Wilaya;

(vii) Kutoza Sh. 5,000 kwa kila kibali cha kusafirisha chakula cha Wanyama ndani na nje ya Wilaya;

(viii) Kutoza kibali kwa ajili ya huduma kwa mifugo na mazao yake wanaopita nchini kwenda nchi nyingine.

Dk. Mpango amependekeza, kufuta tozo mbalimbali kwenye Sekta ya Uvuvi kama

ifuatavyo:

(i)     Kufuta tozo ya mrabaha wa dola za Marekani 0.4 kwa kilo ya samaki katika uvuvi wa bahari kuu;

(ii) Kupunguza ada za leseni ya kuuza samaki na mazao ya uvuvi yanayovuliwa kwenye maji baridi (maziwa, mabwawa na mito) nje ya nchi.

(iii) Kupunguza ada za leseni ya kuuza samaki na mazao ya uvuvi yanayovuliwa kwenye maji chumvi (bahari) nje ya nchi

 (iv) Kupunguza tozo za mrabaha wa kusafirisha samaki nje ya nchi

(v) Kuongeza ada ya leseni ya kuuza Mapezi /taya za papa nje ya nchi kutoka dola za kimarekani 2,700 hadi dola za kimarekani 5,000 kwa ajili ya kuendelea kuhifadhi papa na jamii zake ambao wako hatarini kutoweka;

(vi) Kutoza ada ya leseni ya kusafirisha aina nyingine ya mabondo na makome nje ya nchi

(vii) Kutoza ada ya cheti cha afya ya samaki na mazao yake yanayosafirishwa nje ya nchi (QA/APP/02) Sh. 30,000/= kwa ajili ya kukidhi matakwa ya soko la nje na afya ya mlaji;

(viii) Kutoza tozo za vibali vipya vya kusafirisha samaki na mazao yake

Saba, Dk. Mpango amependekeza kufanya mabadiliko ya tozo za viingilio na huduma 121 mbalimbali zinazotolewa na Makumbusho ya Taifa kama.

Amesema, lengo la mabadiliko haya ni kuongeza Mapato ya Serikali kwa kuwa viwango vinavyotumika sasa ni vya toka mwaka 2002.

Nane, Mabango na Matangazo, Dk. Mpango amesema, “napendekeza kufanya marekebisho kwenye Jedwali la viwango vya tozo chini ya Kanuni za Ada ya Mabango na Matangazo [Local Government Finance (fees for Billboards, Posters and Hoarding) Order 2019], ili kupunguza kiwango cha tozo ya matangazo kwenye magari ya wazalishaji wa bidhaa yanayotumika kusafirisha bidhaa hizo toka viwandani kwenda kwa wasambazaji kutoka kiwango cha sasa cha Sh. 10,000 hadi Sh. 4,000.”

“Lengo la mabadiliko haya ni kukidhi maombi ya wazalishaji dhidi ya tozo hii iliyosababisha wazalishaji wa bidhaa kuondoa matangazo kwenye magari hayo hivyo kupunguza mapato ya Serikali kutoka kwenye chanzo hicho,” amesema

Dk. Mpango amesema, “hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh. 1.25 bilioni.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

error: Content is protected !!