WATANZANIA wametakiwa kutotumia uchaguzi kuwa wakati wa mavuno ya pesa na mali kutoka kwa wagombea, kwani kitendo hicho kinachangia nchi kupata viongozi wasiofaa kutokana na vitendo vya rushwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Wito huo ulitolewa Jana Jumatano na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, katika semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kujadili namna ya kudhibiti rushwa wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
“Watanzania tunapokwenda kwenye uchaguzi tusishiriki vitendo vya rushwa, wapo watanzania wanahisi wakati wa uchaguzi ni wa kuvuna kitendo hiki kinafanya wapatikane viongozi wasiofaa, wasiokuwa na mchango wa maendeleo ya nchi na viongozi mzigo sababu wameingia madarakani kwa rushwa,” alisema Olengurumwa.
Aidha, Olengurumwa alisema TAKUKURU imeamua kutoa semina kwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) na asasi za kiraia kwa kuwa zinajua mchango wake katika utoaji elimu wakati wa uchaguzi na pia ziko nchi nzima.
Olengurumwa alisema THRDC imeanza kazi ya kutoa elimu ya uraia kwa wananchi kuhusu masuala ya uchaguzi, hasa juu ya namna ya kudhibiti rushwa kwa kuwaeleza athari zake katika ukuzaji wa maendeleo yao na nchi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la NGO’s, Dk. Lilian Badi, alisema mashirika hayo yatashirikiana na TAKUKURU katika kudhibiti vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi.
Leave a comment